IQNA

12:31 - December 21, 2020
Habari ID: 3473478
TEHRAN (IQNA) – Wizara ya Afya ya Yemen imetangaza kuwa, watoto wachanga 100,000 hufariki kila mwaka nchini humo punde baada ya kuzaliwa kutokana na vita vinavyoendelea vya Saudia dhidi ya nchi hiyo masikini zaidi katika Bara Arabu.

Naibu Katibu wa Wizara ya Afya ya Yemen Najeeb al-Qubati ameyasmea hayo Jumamosi na kuongeza kuwa, kila masaa mawili watoto sita wa Yemen hupoteza maisha kutokana na athari mbaya za vita vya Saudia dhidi ya Wayemen.

Ameongeza kuwa, utawala wa Saudia umekuwa ukizuia vifaa vya tiba kuingia nchini humo tokea mwaka 2015 wakati ilipoivamia Yemen kijeshi.

Hayo yanajiri wakati ambao Maisha ya mapacha waliozaliwa wakiwa wameunganika Yemen yako hatarini kutokana na mzingiro uliowekwa na Saudi Arabia dhidi ya nchi hiyo.

Katika tukio nadra kujiri kwa mara ya pili nchini Yemen katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, mapacha walio ungana wamezaliwa hivi karibuni katika hospitali ya Al Sabeen, katika mji mkuu wa Yemen, Sana'a.

Watoto hao ambao wako hali mahututi wanaweza kupata matibabu tu nje ya Yemen lakini hilo haliwezekani kutokana na mzingiro wa angani, ardhi na nchi kavu uliowekwa dhidi ya nchi hiyo na Saudia ambayo imeivamia kijeshi nchi hiyo masikini zaidi katika Bara Arabu.

Madaktari katika mji mkuu wa Yemen Sanaa, wametoa ombi la dharura la kuokoa maisha ya mapacha wawili waliozaliwa siku ya Jumatano wakiwa wameunganika.

Mkurugenzi wa hospitali ya Al-Sabeen Majda al-Khatib amesema "Uchunguzi wa kimatibabu umeonesha kuwa mapacha hao wameunganika lakini kila mmoja ana moyo wake, lakini moyo wa mmoja wao uko katika hali ambayo sio hali ya kawaida." 

Hivi karibuni   Henrietta Fore Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), alisema  Yemen ni sehemu hatari zaidi kwa watoto duniani.  Aliongeza kuwa: “Mtoto mmoja hufariki Yemen kila dakika 10 kutokana na magonjwa yanayoweza kuepukika.

Mapema mwezi huu wa Disemba,  Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilitangaza kuwa vita vya Saudi Arabia dhidi ya Yemen vimepelekea zaidi ya watu 233,000 kupoteza maisha katika kipindi cha miaka sita iliyopita.

Ikumbukwe kuwa mnamo mwezi Machi 2015 Saudi Arabia, ikiungwa mkono na  Marekani, utawala haramu wa Israel, Umoja wa Falme za Kiarabu  na nchi zingine kadhaa iliivamia kijeshi Yemen na kuiwekea mzingiro wa kila upande.

Utawala dhalimu wa Saudia ulianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha madarakani kibaraka wake, Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh. Hata hivyo hadi sasa Saudia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao kutokana na kusimama kidete wananchi wa Yemen.

3473460

Kishikizo: yemen ، watoto ، saudia
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* captcha: