IQNA

Italia yapiga marufuku uuzaji silaha kwa Saudia, UAE kutokana na jinai zao Yemen

16:08 - January 30, 2021
Habari ID: 3473603
TEHRAN (IQNA)- Italia imetangaza kusitisha uuzaji silaha zake kwa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kutokana na jinai za kivita ambazo tawala hizo mbili zinafanya huko Yemen.

Katika taarifa jana Ijumaa, Luigi Di Maio, Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia alisema, "hii ni hatua tuliyoafikia kuwa ya dharura na ujumbe wa wazi kutoka nchi hii. Kwetu sisi, kuheshimu haki za binadamu ni wajibu usiovunjika."

Harakati za kupinga mauzo ya silaha kwa Saudia na Imarati chini ya mwavuli wa Italian Peace and Disarmament Network zimepongeza hatua hiyo na kusisitiza kuwa, kitendo hicho kwa uchache kitazuia uuzaji wa mabomu 12,700.

Mwaka 2018, Waziri Mkuu wa Italia, Giuseppe Conte aliahidi kuwa nchi hiyo itasitisha mauzo ya silaha kwa Saudia, kufuatia mauaji ya kikatili ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari aliyekuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Aal-Saud.

Mapema wiki hii, serikali ya Joe Biden ilitagaza kusitisha uuzaji silaha za Marekani kwa Saudia na ndege za kivita aina ya F-35 kwa Imarati. Siku chache kabla ya Biden kuapishwa kuwa rais mpya wa Marekani, Donald Trump, rais wa nchi hiyo aliyemaliza muda wake aliafiki mpango wa kuiuzia Imarati ndege 50 za kivita aina ya F35 zenye thamani ya dola bilioni 23.

Hivi karibuni, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilisema kati ya Januari na Juni 2021, asilimia 54 ya Wayemen, yaani watu milioni 16.2, watakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.

Aidha mwezi Disemba mwaka jana,  Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilitangaza kuwa vita vya Saudi Arabia dhidi ya Yemen vimepelekea zaidi ya watu 233,000 kupoteza maisha katika kipindi cha miaka sita iliyopita.

Ikumbukwe kuwa mnamo mwezi Machi 2015 Saudi Arabia, ikiungwa mkono na  Marekani, utawala haramu wa Israel, Umoja wa Falme za Kiarabu  na nchi zingine kadhaa iliivamia kijeshi Yemen na kuiwekea mzingiro wa kila upande.

Utawala dhalimu wa Saudia ulianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha madarakani kibaraka wake, Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh. Hata hivyo hadi sasa Saudia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao kutokana na kusimama kidete wananchi wa Yemen.

3473834

Kishikizo: yemen ، italia ، silaha ، saudia ، uae
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* :