IQNA

Indhari ya Mufti wa Misri kuhusu njama za Israel za kuuyahudisha mji wa Quds

16:35 - February 27, 2021
Habari ID: 3473687
TEHRAN (IQNA)- Mufti Mkuu wa Misri ametadharisha juu ya njama ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuuyahudisha mji mtukufu wa Quds unaokaliwa kwa mabavu, na kufuta kabisa utambulisho wake halisi.

Sheikh Shawki Allam ametoa indhari hiyo baada ya utawala haramu wa Israel kupiga marufuku kusomwa adhana katika Msikiti wa Ibrahim, kwa kisingizio kuwa walowezi wa Kiyahudi wanasherehekea maadhimisho ya Kiyahudi ya Purim.

Katika taarifa, Mufti Allam amekosoa vikali uvamizi wa mara kwa mara unaofanywa na Wazayuni dhidi ya misikiti ya Palestina hususan Masjidul Aqsa, wakipewa ulinzi na maafisa usalama wa utawala huo khabithi.

Kadhalika Mufti Mkuu wa Misri amelaani vikali kitendo cha Wazayuni kufanya matambiko yao ya Talmudic katika maeneo hayo matakatifu ya Waislamu yanayokaliwa kwa mabavu.

Wakati huohuo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imesema hatua hiyo ya kupigwa marufuku adhana katika Msikiti wa Ibrahim tokea Alkhamisi iliyopita ni sawa na tangazo la vita vya kidini.

Naye Mkurugenzi wa msikiti huo, Sheikh Hefzi Abu Sneina, amesema marufuku hiyo ambayo inatazamiwa kumalizika leo jioni ni ukiukaji wa wazi wa uhuru wa kuabudu, unaolindwa na sheria za kimataifa.

Utawala wa Kizayuni unatekeleza misingi mitatu mikuu ambayo ni kuugawa utumiaji wa Msikiti wa Al Aqsa kisehemu na kiwakati, kuchimba mashimo ya chini kwa chini na kandokando ya msikiti na kuyahudisha maeneo ya jirani na mahala hapo patakatifu.

Hii ni katika hali ambayo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limethibitisha tena kwamba msikiti mtukufu wa Al-Aqsa, kibla cha kwanza cha Waislamu ni milki ya Wapalestina.

3956401

Kishikizo: misri ، quds tukufu ، israel ، palestina ، Shawki Allam
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha