IQNA

Hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Katika Siku ya Kimataifa ya Quds

18:39 - May 07, 2021
Habari ID: 3473886
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, harakati ya kuporomoka na kutoweka utawala wa Kizayuni imeanza na haitasimama; na akawahutubu Mujahidina wa Palestina kwa kuwaambia: "Endelezeni mapambano halali dhidi ya utawala ghasibu ili ulazimike kukubali kura ya maoni."

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo leo katika Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani na kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds.

Ifuatayo ni matini kamili ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu.

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.

Himidi zote ni za Mwenyezi Mungu mlezi wa walimwengu na rehema na amani ziwe kwa mtukufu Muhammad (s.a.w.w), hitimisho la Mitume, mbora wa viumbe wote na Ali zake watoharifu na masahaba wote walio wema na kila aliowafuata kwa wema mpaka siku ya malipo.

Palestina; kadhia muhimu na hai zaidi ya Umma wa Kiislamu

Kwa hakika kadhia ya Palestina, imeendelea kuwa suala muhimu kabisa, hai zaidi la pamoja la Umma wa Kiislamu. Mfumo wa kibeberu na kidhali ulilifukuza taifa kutoka katika nchi  na ardhi ya mababu zake kisha ukaanzisha hapo utawala wa kigaidi na kuwaweka watu ajinabi mahala pake.

Mantiki ya kuasisi utawala wa Kizayuni wa Israel

Ni mantiki gani dhaifu zaidi na isiyo na mashiko kama mantiki tupu (iliyotumiwa) ya kuasisi utawala wa Kizayuni wa Israe?

Madola ya Ulaya kama yanavyodai ni kuwa, ziliwadhulumu Mayahudi katika miaka ya kujiri Vita Vikuu vya Pili vya Dunia basi kuna ulazima wa kisasi cha Mayahudi (hao) kilipizwe kwa kuwafanya wakimbizi watu wa taifa moja katika Asia Magharibi na kwa mauaji ya kinyama ndani ya nchi hiyo. Kwa kufanya hivyo, zimeyabatilisha madai yao ya uongo kuhusu haki za binadamu na demokrasia…!

Hii ndio mantiki iliyotegemewa na madola ya Magharibi kwa ajili ya kutoa himaya  ya kila upande na ya kiwendawazimu kwa utawala wa Kizayuni na kwa msingi huo, kuwa tayari kutoa madai yao ya uongo kuhusiana na haki za binadamu na demokrasia. Na kichekesho na kitendo hiki cha kuliza kinaendelea kwa miaka 70 sasa, na kila baada ya muda huongezwa karatasi jingine katika kadhia hiyo.

Mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni ni jukumu la wote

Wazayuni wameighusubu Palestina na kuanzia siku ya kwanza waliibadilisha kuwa kambi na kituo cha ugaidi. Israel sio nchi, bali ni kituo cha ugaidi dhidi ya taifa la Palestina na mataifa mengine ya Waislamu. Kupambana na utawala huo mmwagaji damu, ni kupambana na dhulma na ugaidi na hili ni jukumu la wote.

Udhaifu na mifarakano katika umma wa Kiislamu, imeandaa mazingira ya kughusubiwa Palestina

Nukta ya kuzingatiwa ni hii kwamba, ingawa serikali ghasibu iliundwa mwaka 1948 lakini utangulizi wa kuteka sehemu hii hasasi katika eneo la Kiislamu ilianza miaka mingi nyuma. Miaka hiyo ilisadifiana na uingiliaji amilifu wa Magharibi katika nchi za Kiislamu kwa ajili ya kuhakikisha usekula unatawala sambamba na utaifa wenye kufurutu ada na pofu na halikadhalika kuleta madarakani serikali za kidekteta ambazo ni tegemezi au vibaraka wa Magharibi.

Utafiti kuhusu zama hizo nchini Iran na Uturuki na nchi za Kiarabu za Asia Magharibi hadi Afrika Kaskazini unabaini ukweli huu mchungu kuwa, udhaifu na mifarakano  katika umma wa Kiislamu ni jambo ambalo liliandaa mazingira ya kujiri maafa ya kughusubiwa Palestina na hilo ni pigo ambalo umma wa Kiislamu umepata kutoka kwa ulimwengu wa Kiistikbari.

Muungano wa kambi za Magharibi na Mashariki na mabepari wa Kizayuni dhidi ya Palestina

Somo ambalo tunapata leo ni hili kuwa, katika zama hizo, kambi zote za Ubaperi na Ukomunisti ziliweza kushirikiana na  Maqaruni wa Kizayuni; njama kuu ilitekelezwa na kufuatiliwa na Uingereza huku mabepari wa Kizayuni wakichukua jukumu la kutoa pesa na silaha kwa ajili ya kutekeleza njama hiyo. Shirikisho la Sovieti nalo lilikuwa serikali ya kwanza ambayo ilitambua rasmi serikali haramu ambayo ilikuwa imeasissiwa na kisha ikawapeleka Mayahudi wengi katika eneo hilo.

Kwa upande mmoja, utawala ghasibu ni matokeo ya hali ya wakati huo katika ulmwengu wa Kiislamu na kwa upande wa pili njama hii ya kuhujumu na kuvamia ilitekelezwa na Ulaya.

Mabadiliko katika mlingano wa nguvu kwa maslahi ya ulimwengu wa Kiislamu

Leo hali ya dunia si kama ilivyokuwa katika siku hizo; na huu ni ukweli ambao daima tunapaswa kuuzingatia. Leo mlingano wa nguvu umebadilika kwa maslahi ya Uislamu. Matukio mbali mbali ya kisiasa na kijamii Ulaya na Marekani, udhaifu na mvurugiko wa kina katika muundo, usimamizi na maadili ya Magharibi ni mambo ambayo yamewaanika wazi Wamagharibi mbele ya walimwengu.  Mwaka moja wa Marekani na Ulaya kushindwa  kukabiliana na janga la corona na mambo mengine ya kuaibisha yaliyoandamana na janga hilo, pamoja na mvuruguko wa hivi karibuni wa kisiasa na kijamii katika nchi muhimu zaidi za Ulaya, yote ni mambo ambayo yanaonyesha kuanza kuchukua mkondo ya  kusambaratika kambi ya Magharibi.

Katika upande mwingine, kuimarika vikosi vya muqawama katika maeneo nyeti mno ya Kiislamu, kuimarika uwezo wao wa kiulinzi na kimashambulizi, kuimarika na kuongezeka kujielewa na kupata msukumo na matumaini zaidi mataifa ya Waislamu, kuimarika hamu ya kushikamana na kaulimbiu za Kiislamu na Qur'ani, kustawi kielimu, kupata nguvu fikra ya kupenda uhuru, ukombozi na kujitegemea mataifa ya dunia, yote hayo ni ishara nzuri zinazotoa bishara ya mustakbali bora.

Umuhimu wa kushirikiana Waislamu katika mhimili wa Palestina na Quds

Katika mustakbali huo wenye baraka, lazima suala la ushirikiano na kushikamana nchi za Waislamu liwe lengo kuu na la kimsingi, na jambo hilo si gumu sana kupatikana. Mhimili wa ushirikiano na mshikano huo ni kadhia ya Palestina kwa maana ya nchi yote na mustakbali wa Quds tukufu. 

Ushirikiano baina ya Waislamu katika mhimili wa Quds Tukufu ni jinamizi kwa adui Mzayuni na waungaji mkono wake wa Marekani na Ulaya. Mpango uliofeli wa "Muamala wa Karne" na baadaye njama za kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala huo ghasibu zilizofanywa na nchi kadhaa dhaifu za Kiarabu, ni juhudi zilizofeli za kujipapatua kutoka katika jinamizi hilo.

Ninasema kwa imani thabiti kwamba, juhudi zao zote hizo hazitofanikiwa. Harakati ya kuporomoka na kuangamia utawala adui wa Kizayuni imeanza na haitokwama.

Uungaji mkono wa Waislamu wa dunia kwa wanajihadi wa Palestina

Sababu mbili ni muhimu mno katika kuainisha mustakbali bora: Sababu ya kwanza na ambayo ndiyo muhimu zaidi, ni kuendelea muqawama ndani ya radhi za Palestina na kutiwa nguvu utamaduni na fikra ya jihadi na kufa shahidi na sababu ya pili ni uungaji mkono wa kimataifa wa tawala na wananchi Waislamu kote ulimwenguni, kwa wanajihadi wa Palestina.

Watu wote - watawala, wanafikra, maulamaa wa kidini, vyama na makundi mbalimbali, vijana wenye ghera na matabaka mengine yote - wote kwa pamoja tunapaswa tuwe na nafasi yetu na tutekeleze vizuri majukumu yetu katika harakati hii ya dunia nzima. Ni kwa njia hii ndipo itawezekana kuvunja njama za adui na ni wakati huo ndipo itatimia ahadi ya Mwenyezi Mungu iliyomo kwenye aya inayosema: أَمْ یُرِیدُونَ کَیْدًا فَالَّذِینَ کَفَرُوا هُمُ الْمَکِیدُونَ Au wanataka kufanya vitimbi tu? Lakini hao waliokufuru ndio watakaotegeka, ahadi ambayo ni moja ya matukio ya Zama za Mwisho (Aakhiruz Zaman) na وَاللَّهُ غَالِبٌ عَلَى أَمْرِهِ وَلَکِنَّ أَکْثَرَ النَّاسِ لاَ یَعْلَمُونَ Na Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye kushinda katika jambo Lake, lakini watu wengi hawajui.

 

Ifuatayo hapa chini ni tarjama ya Kiswahili ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, aliotoa kwa lugha ya Kiarabu.

 

Napendelea pia kuzungumza kidogo na vijana wa Kiarabu kwa kutumia lugha yao wenyewe: Salamu za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya Waarabu wote huru hususan vijana. Salamu ziwe juu ya wanamapambano wa Palestina na Quds walioko lindoni huko Masjidul Aqsa.

 

Bismillahir Rahmanir Rahiim.

Sala na Salamu za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya Bwana wetu Muhmmad, Mtume wa mwisho na mbora wa viumbe wote. Na pia ziwashukie Aali zake watoharifu, Masahaba zake wema na wafuasi wao kwa wema hadi siku ya Kiayama. Hakika kadhia ya Palestina ingali kadhia muhimu ya pamoja ya Umma ya Kiislamu na iliyohai zaidi. Mfumo wa kibepari na kidhali ulilifukuza taifa zima kwenye nchi yake na kuanzisha utawala wa kigaidi na kuwaweka watu ajnabi mahala pake.

Mashahidi wa muqawama

Salamu za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya mashahidi wa Muqawama na wapiganaji Jihadi wengi waliosabilia uhai wako katika njia hii hususan Shahidi Sheikh Ahmad Yasin, Shahidi Sayyid Abbas Mousawi, Sahidi Fathi Shaqaqi, Shahidi Imad Mughniya, Shahidi Abdul Azizi Rantisi na Shahidi Abu Mahdi al Muhandis, na hatimaye sura inayong'aa ya mashahidi wa Muqawama, Shahidi Qassem Soleimani; ambao kila mmoja wao na baada ya uhai na maisha yaliyojaa matunda na baraka, ameacha taathira kubwa katika mazingira ya Muqawama na mapambano kutokana na kuuliwa kwake shahidi. 

Jihadi ya Wapalestina na damu safi ya mashahidi wa Muqawama na mapambano imeendelea kupeperusha bendera ya hii yenye baraka na kuzidisha mara mamia kadhaa uwezo wa jihadi ya ndani ya Palestina. Wakati mmoja kijana wa Kipalestina alikuwa akijihami wa kurusha jiwe, na hii leo anajibu hujuma ya adui kwa kurusha kombora linalolenga shabaha kwa umakini mkubwa. 

Ardhi Takatifu

Palestina na Quds imetajwa katika Qur'ani tukufu kuwa ni "ardhi takatifu". Kwa miongo kadhaa sasa ardhi hiyo tukufu inakaliwa kwa mabavu na watu wachafu zaidi na wanadamu habithi kuliko wote. Inakaliwa kwa mabavu na mashetani wanaowaua kikatili watu sharifu na kisha wanakiri kifidhuli kufanya mauaji hayo. Quds inakaliwa kwa mabavu na wabaguzi wa rangi ambao kwa zaidi ya miaka sabini sasa wanawanyanyasa wamiliki asili wa ardhi hiyo kwa kuwaua, kupora mali zao, kuwafunga jela na kuwatesa. Hata hivyo, kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu, hawajafanikiwa kuvunja irada na azma yao. 

Palestina iko hai na inaendeleza mapambano ya Jihadi, na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, hatimaye itamshinda adui muovu. Quds tukufu na ardhi yote ya Palestina ni mali ya watu wa Palestina na itarejea kwao, inshaallah, kwani "jambo hilo si gumu kwa Mwenyezi Mungu".    

Majukumu ya Waislamu

Nchi na mataifa yote ya Waislamu yana wajibu na majukumu ya kufanya kuhusiana na kadhia ya Palestina. Hata hivyo nguzo kuu ya Muqawama na mapambano ni Wapalestina wenyewe ambao hii leo wanakaribia milioni 14 ndani na nje ya ardhi ya Palestina. Umoja na azma kubwa ya idadi hii itaweza kufanya kazi kubwa na adhimu. Hii leo umoja ndiyo silaha kubwa zaidi ya Wapalestina. 

Maadui wa umoja na mshikamano wa Wapalestina ni utawala wa Kizayuni wa Israel, Marekani na baadhi ya makundi ya kisiasa. Hata hivyo iwapo umoja huo hautavunjwa kutokea ndani ya jamii ya Wapalestina wenyewe basi kwa hakika maadui wa nje hwataweza kufanya lolote. Msingi na nguzo kuu ya umoja huo unapaswa kuwa Jihadi ya ndani na kutowategemea na kuwaamini maadui. Adui mkuu wa Wapalestina, yaani Marekani, Uingereza na Wazayuni habithi hawapasi kufanywa egemeo la siasa za Palestina.  

Stratijia ya Umoja

Wapalestina wote, sawa wale walioko Ukanda wa Gaza, au Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan au katika ardhi ya Palestina ya mwaka 1948 na hata wanaoishi kwenye kambi za wakimbizi, wote wanaunda kitu kimoja na wanapaswa kuweka mbele stratijia ya kuungana. Kila sehemu moja inapaswa kuihami na kuitetea sehemu nyingine na kutumia nyenzo zake kutetea sehemu hiyo ya Wapalestina wakati wa mashinikizo. 

Hii leo matumaini ya kupata ushindi ni makubwa zaidi kuliko wakati wowote mwingine, na mlingano wa nguvu umebadilika sana kwa maslahi ya Wapalestina. Adui Mzayuni anadhoofika zaidi mwaka baada ya mwingine na jeshi lake alilolitaja kuwa ni "jeshi ambalo kamwe halishindiki", hii leo limekuwa "jeshi ambao kamwe halitaonja tamu ya ushindi" baada ya tajiriba ya vita vya siku 33 huko Lebanon na tajiriba ya vita vya siku 22 na siku 8 katika Ukanda wa Gaza. Hali mbaya ya kisiasa ya utawala huo ambao umelazimika kuitisha chaguzi nne za Bunge katika kipindi cha miaka miwili, hali yake mbaya ya kiusalama ya kushindwa mtawalia, na hamu kubwa ya Wayahudi ya kuhajiri na kukimbia Israel, yote hayo ni kielelezo cha fedheha kwa utawala huo wenye majigambo mengi.

Israel kuanzisha uhusiano na Waarabu

Jitihada kubwa za utawala huo za kutaka kuanzisha uhusiano wa kawaida na nchi kadhaa za Kiarabu kwa msaada wa Marekani ni kielelezo kingine cha udhaifu wa utawala huo ghasibu. Pamoja na hayo jitihada hizo pia zitagonga mwamba. Miongo kadhaa iliyopita utawala wa Kizayuni wa Israel ulianzisha uhusiano na Misri, tangu wakati huo utawala huo umekuwa tete na kudhoofika zaidi. Kwa msingi huo, je kuanzisha uhusiano na nchi kadhaa dhaifu na duni kutausaidia kitu utawala huo? Nchi hizo pia hazitafaidika na uhusiano huo. Adui Mzayuni atatumia mali au ardhi yao na kueneza uharibifu na ukosefu wa usalama baina yao. 

Ukweli huu haupaswi kutusahaulisha majukumu mazito ya pande nyingine kuhusiana na harakati hii. Maulama wa Kiislamu na Kikristo wanapaswa kuitambua hatua yoyote ya kuanzisha uhusiano na Israel kuwa ni haramu, na wanafikra na watu huru wabainishe na kuweka wazi matokeo mabaya ya jinai hiyo ambayo ni sawa na kuisaliti Palestina. 

Kuporomoka Israel

Katika upande mwingine mwenendo wa kuporomoka utawala wa Kizayuni na kuongezeka uwezo wa kambi ya mapambano, kuongezeka uwezo wa kiulinzi na kijeshi, kujitosheleza katika utengenezaji wa silaha athirifu, hali ya kujiamini ya wanajihadi, kujitambua kunakoongezeka baina ya vijana, kupanuka zaidi muqawama na mapambano katika nchi yote ya Palestina, na mwamko na hivi karibuni wa vijana katika kulinda Msikiti wa al Aqsa na kuakisiwa Jihadi sambamba na kudhulumiwa taifa la Palestina katika fikra za watu katika maeneo mengi ya dunia, ni bishara ya mustakbali unaong'aa.  

Mantiki ya Wapalestina

Mantiki ya mapambano ya Wapalestina pia ambayo imesajiliwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyaraka za Umoja wa Mataifa, ni mantiki aali na yenye kuvutia. Wanamapambano wa Kipalestina wanaweza kuitisha kura ya maoni baina ya wakazi wote asili wa Palestina. Kura hiyo ya maoni itaainisha mfumo wa kisiasa wa nchi, na wakazi asilia wa kila kaumu na dini, wakiwemo wakimbizi wa Kipalestina watashirikisha katika kura hiyo. Mfumo huo wa kisiasa utawarejesha wakimbizi ndani ya nchi yao na utaainisha hatima ya wageni waliopewa makazi katika ardhi ya Palestina.   

Takwa hili limetolewa kwa mujibu wa misingi ya demokrasia ya sasa ambayo imekubalika duniani, na hakuna mtu anayeweza kutia dosari katika ubora wake. Wanamapambano wa Palestina wanapaswa kudumisha kwa nguvu zote mapambano yao halali na ya kimaadili dhidi ya utawala ghasibu hadi utakapokubali matakwa haya. Pigeni hatua kuelekea mbele kwa jina la Mwenyezi Mungu, na eleweni kwamba "Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anayemsaidia Yeye".

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

3969852

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* :