IQNA

Kiongozi wa HAMAS amwandikia barua Kiongozi Muadhamu kuhusu yanayojiri Quds

14:44 - May 10, 2021
Habari ID: 3473894
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amemwandikia barua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kumjulisha matukio na mabadiliko yanayojiri katika mji wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu.

Katika barua hiyo kwa Ayatullah Sayyid Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Ismail Haniya Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas ametaka Ulimwengu wa Kiislamu uchukue msimamo madhubuti katika kuwaunga mkono wakazi wa mji huo mtukufu na kukomesha jinai za utawala ghasibu wa Israel.

Aidha  amesisitiza kuwa, hujuma na uvamizi wa Wazayuni dhidi ya Quds tukufu na eneo la Babul-A'muud na Sheikh Jarrah; na vilevile uvamizi dhidi ya msikiti wa Al Aqsa na waliokaa itikafu ndani yake ni njama kubwa zinazofanywa na viongozi wa utawala vamizi na ghasibu kwa ajili ya kuhalalisha ujenzi wa vitongoji, kuwahamisha Wapalestina kwa nguvu, kuwanyang'anya nyumba zao na kuuzatiti mpango wa kuugawa msikiti huo kieneo na kiwakati katika utumizi wake, pamoja na kuibadilisha hali yake ya hivi sasa.  

Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas amebainisha kuwa, jinai za utawala zimekwenda mbali zaidi na kuvuka mistari myekundu yote na kuzijeruhi hisia za umma za Kiislamu, mbali na kuulenga na kuuhujumu mji wa Quds, historia yake ya Kiislamu, utambulisho wake, njia za kupatia riziki, mustakabali na haki za kisheria za wakazi wa mji huo; kama ambavyo zimeulenga pia moja kwa moja msikiti wa Al Aqsa na waliojitolea kuulinda.

Katika barua yake hiyo kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ismail Haniya ametoa mwito kwa Ulimwengu wa Kiislamu kuonyesha harakati ya haraka kwa kuchukua msimamo madhubuti kuhusiana na jinai za utawala wa Kizayuni na kufanya jitihada za uhamasishaji kwa ajili ya kupatikana msimamo wa pamoja wa Kiislamu, diplomasia ya pamoja ya Kiarabu, Kiislamu na kimataifa kwa madhumuni ya kumzuia adui Mzayuni asiendeleze jinai zake za kinyama dhidi ya wananci wa Palestina, ardhi hiyo na matukufu yake katika mji unaokaliwa kwa mabavu wa Quds na hasa msikiti uliobarikiwa wa Al Aqsa.

Wapalestina wapatao 90,000 walisali katika msikiti wa Al Aqsa usiku wa kuamkia leo, ukiwa ni mmoja wa mikesha inayotajwa kuwa yumkini ukawa wa Lailatul-Qadr, ambapo katika makabiliano yaliyosababishwa na hujuma za askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel, waumini wasiopungua 90 walijeruhiwa.

3474666/

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha