IQNA

Vita vya Saudia dhidi ya Yemen vimeua watoto zaidi ya 4000

22:36 - July 13, 2021
Habari ID: 3474097
TEHRAN (IQNA)-Kituo cha sheria mjini Sana'a kimetoa takwimu za jinai zilizofanywa na muungano wa Saudi Arabia katika kipindi cha siku 2,300 za uvamizi wake nchini Yemen.

Kituo cha sheria na maendeleo cha A'inul-Insaaniyyah kilichoko mji mkuu wa Yemen Sana'a kimetangaza kuwa, idadi ya wahanga wa jinai zilizofanywa na muungano wa Saudia katika muda wa siku 2,300 zimefika watu 43,891 waliouawa shahidi na waliojeruhiwa, kwa upande wa raia wa kawaida.

Kituo hicho kimeongeza kuwa, katika kipindi hicho cha vita, raia 17,176  wakiwemo watoto 3,842 na wanawake 2,400 wameuawa na wengine 26,715 wakiwemo watoto 4,225 na wanawake 2,832 wamejeruhiwa.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, idadi ya taasisi zilizobomolewa nchini Yemen zimefikia 10,496. Kadhalika, hujuma na mashambulio yaliyofanywa na muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia yamesababisha hasara kwa viwanja vya ndege 15, bandari 16, vinu 308 vya umeme na mitandao 553 ya mawasiliano, mbali na kuteketeza na kuharibu maghala na mitandao ya usambazaji maji 2,397, vituo 1,983 vya serikali na madaraja 5,224.

Mashambulio ya wavamizi dhidi ya Yemen yameharibu na kusababisha hasara pia kwa taasisi 23,665 za kiuchumi, viwanda 396, meli 352 za mafuta, taasisi 11,479 za kibiashara na vituo 423 vya ufugaji kuku.

Vituo 179 vya vyuo vikuu, misikiti 1,446, hospitali na vituo vya afya 391 na skuli na vituo vya elimu 1,110 vimeharibiwa pia katika hujuma na mashambulio hayo.

Uvamizi na mashambulio ya Saudi Arabia na waitifaki wake dhidi ya Yemen yaliyoanzishwa Machi 2015 yameshaingia katika mwaka wa saba.

3475226/

Kishikizo: yemen watoto saudia
captcha