IQNA

Yemen inakabiliwa na baa kubwa la njaa, Saudia yaendeleza hujuma

16:37 - February 19, 2021
Habari ID: 3473663
TEHRAN (IQNA)- Yemen inakabiliwa na baa kubwa la njaa ambalo linaweza kuvuruga jitihada mpya za kusaka amani katika nchi hiyo ambayo kwa miaka sita sasa imekuwa ikikabiliwan na hujuma ya kijeshi ya Saudi Arabia na waitifaki wake,

Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen Martin Griffiths ametoa tahadhari hiyo Alhamisi huku akitaka pande hasimu zisitishe mapigano.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kibinadamu jana aliitaja hali ya kibinadamu huko Yemen kuwa ya maafa na kutangaza kuwa, hivi asa kuna karibu watoto laki nne chini ya miaka mitano wenye utapiamlo nchini humo.

Mark Lowcock amesema kuwa, Yemen inaelekekea kwa kasi katika hali mbaya ya maafa makubwa sana ya njaa yaliyowahi kushuhudiwa duniani katika miongo kadhaa iliyopita na kwamba karibu dola bilioni 4 zinahitajika sasa ili kutekeleza oparesheni za kibinadamu huko Yemen na kuzuia njaa nchini humo.  

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF), Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Shirika la Afya Duniani (WHO) pia hivi karibuni yalitoa ripoti na kueleza kuwa, watoto wa Kiyemen laki nne walio na umri chini ya miaka mitano wako katika hatari ya kifo kutokana na njaa inayowakabili. 

Mashirika hayo manne ya Umoja wa Mataifa yamesema kuwa, Yemen inakabiliwa na mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu duniani na kutaka kufikishwa misaada ya kibinadamu kwa raia wa Yemen bila kizuizi. Uvamizi na vita vinavyoendelea kufanywa na muungano vamizi wa Saudia huko Yemen umepelekea nchi hiyo maskini ya Kiarabu kukumbwa na uhaba mkubwa wa chakula na dawa za matibabu. 

Utawala dhalimu wa Saudia ulianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mnamo Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha madarakani kibaraka wake, Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh. Hata hivyo hadi sasa Saudia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao kutokana na kusimama kidete wananchi wa Yemen wakiongozwa na Harakati ya Ansarullah. Harakati hiyo imekuwa ikitekeleza mashambulizi ya kulipiza kisasi ndani ya ardhi ya Saudi Arabia ambapo imeleng mara kadhaa vituo vya kusafisha mafuta na pia viwanja vya ndege vinavyotumiwa na jeshi vamizi la utawala huo wa kifalme.

Hivi karibuni, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilisema kati ya Januari na Juni 2021, asilimia 54 ya Wayemen, yaani watu milioni 16.2, watakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula kutokana na vita vya Saudia dhidi ya nchi hiyo.

Aidha mwezi Disemba mwaka jana,  Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilitangaza kuwa vita vya Saudi Arabia dhidi ya Yemen vimepelekea zaidi ya watu 233,000 kupoteza maisha katika kipindi cha miaka sita iliyopita.

3474020/

captcha