IQNA

Al-Wefaq yalaani hatua za utawala Bahrain dhidi ya maombolezo ya Muharram

22:03 - August 22, 2021
Habari ID: 3474217
TEHRAN (IQNA) Kundi kuu la upinzani la Bahrain, Jumuiya ya Kitaifa ya Kiislamu ya al-Wefaq, imelaani mashambulio na uchokozi wa utawala Al Khalifa wakati wa maombolezo ya Muharram.

Al-Wefaq katika taarifa yake imelaani vitendo vya uchochezi vya vikosi vya usalama vya utawala huo wa kifalme dhidi ya wale wanaokumbuka kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad SAW,  Imam Hussein AS

Ilisema hatua kama hizo zinaashiria kina na ukubwa wa mzozo wa kisiasa nchini na ukosefu wa utulivu wa amani kati ya watawala na wananchi. Taarifa hiyo ilibainisha kuwa wakati wa siku kumi za kwanza za Muharram, vikosi vya usalama vya serikali viliita na kuwahoji wasomi wa Kishia, wahubiri, maafisa wa vituo vya kidini, malenga, na watu wengine kwa lengo la kuwadhalilisha kwa kushiriki katika vikao vya kidini.

Pia maafisa wa usalam walirarua na kuangusha mabango na bendera za Ashura katika maeneo tofauti ya Bahrain, ilisema taarifa hiyo.

Al-Wefaq imeilaani vikali serikali kwa kutumia janga la corona kama njia ya kulazimisha kuzuia shughuli za kidini.

Kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita, mwaka huu pia utawala wa kifamilia wa Aal Khalifa nchini Bahrain umepiga marufuku kufanya shughuli zozote zile za Waislamu wa madhehebu ya Kishia za maombolezo ya Muharram na kumbukumbu ya kifo cha Imam Hussein AS

Kwa akali asilimia 65 ya wananchi wa Bahrain ni Mashia. Licha ya kuwa Mashia ndio wanaounda asilimia kubwa ya wananchi wa Bahrain, lakini hawapati hata haki za watu walio wachache, na badala yake wamekuwa chini ya dhulma na ukandamizaji mkubwa tena wa kuratibiwa unaofanywa na utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifa.

Miongoni mwa haki za Mashia wa Bahrain zinazokanyangwa na utawala wa nchi hiyo ni haki za kimadhehebu. Ukweli ni kuwa, ubaguzi wa kimadhehebu ni sehemu ndogo tu ya mamia ya haki za Mashia zinazokiukwa na utawala wa Aal Khalifa nchini Bahrain.

Suala hilo hudhihirika zaidi unapowadia mwezi wa Muharram. Waislamu wa Kishia nchini Bahrain kama walivyo Mashia wengine ulimwenguni wanatambua kuwa, kufanya maombolezo ya Imam Hussein katika mwezi wa Muharram ni mambo ya kupewa kipaumbele ambayo haiwezekani kutoyafanya.

Pamoja na hayo, utawal wa Aal Khalifa hauko tayari kuvumilia na kuwaacha Mashia wafanye marashimu hayo ya kimadhehebu. Kwa muktadha huo, kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita, mwaka huu pia vyombo vya usalama vya Bahrain vimekwenda katika miji na mitaa mbalimbali ya nchi hiyo na kuendeleza mbinu za ukandamizaji za utawala wa Aal Khalifa kwa kukusanya bendera na mabango yote yenye nembo za kumbukumbu ya Muharram.

3992072

Kishikizo: bahrain muharram shia
captcha