IQNA

Wizara ya Wakfu Syria yakanusha kufunga Haram ya Bibi Zaynab (SA) au kuzuia maombolezo ya Muharram

18:52 - June 29, 2025
Habari ID: 3480869
IQNA – Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kidini nchini Syria imekanusha taarifa zilizosambaa mitandaoni na kwenye vyombo vya habari kuwa Haram takatifu ya Bibi Zaynab (Salamullahi ‘alayha) mjini Damascus imefungwa.

Taarifa hizo za awali zilidai kuwa eneo hilo la ibada limefungwa, na kuwa maombolezo ya kumbukumbu ya kuuliwa kwa Imam Hussein (Alayhis Salaam) yamepigwa marufuku katika mwezi mtukufu wa Muharram.

Ofisi ya habari ya wizara hiyo imetoa ufafanuzi kuwa eneo hilo liko wazi kwa wafanyaziara na kwamba hakuna marufuku yoyote juu ya kufanya maombolezo au shughuli za kidini katika siku za Ashura au Muharram kwa ujumla.

Wizara imesisitiza kuwa inaendelea kuunga mkono shughuli za ziara kwa maeneo matukufu nchini Syria kwa waumini wote, na inafanya juhudi kuhakikisha maandalizi ya kiusalama ili kuwalinda wageni wa maeneo hayo ya ibada.

Picha zilizosambazwa mitandaoni zimeonesha maadhimisho yaliyofanyika usiku wa kwanza wa Muharram katika Haram au kaburu takatifu la Bibi Zaynab (SA), ambapo waumini kadhaa walihudhuria kwa ajili ya dhikri na maombolezo.

Tangu kuongezeka kwa ushawishi wa kundi la Hay’at Tahrir al-Sham (HTS) nchini Syria mnamo Oktoba 2024, kaburi la Bibi Zaynab (SA) limekuwa ikikumbwa na changamoto mbalimbali.

Licha ya msimamo mkali wa Kiwahhabi wa HTS dhidi ya maeneo ya Waislamu wa madhehebu ya Shia, kundi hilo linalotawala Syria limeahidi kwamba litachukua tahadhari kubwa kuhusiana na maeneo hayo matukufu, hasa maeneo matakatifu ya Kishia, ili kuepusha uchokozi wowote wa kimadhehebu ambao unaweza kuchochea hasira ya umma.

Waislamu wa Kishia pamoja na Waislamu wengine kote ulimwenguni huadhimisha kila mwaka kumbukumbu ya kuuawa shahidi kwa Imam Hussein (AS) katika mwezi wa Muharram.

Imam Hussein (AS), ambaye ni Imamu wa Tatu katika mfululizo wa Maimamu wa Ahlul Bayt, pamoja na watu wa familia na wafuasi wake, waliuawa shahidi katika vita vya Karbala mnamo tarehe 10 Muharram (Ashura), mwaka 61 Hijria kwa mikono ya jeshi la Yazid bin Muawiya.

Kwa mwaka huu wa 2025, Siku ya Ashura itasadifu Jumapili, tarehe 6 Julai.

3493634

captcha