IQNA

Watu wa Bahrain wapinga safari ya waziri wa utawala wa Israel katika nchi yao

14:10 - October 01, 2021
Habari ID: 3474366
TEHRAN (IQNA)- Watu wa Bahrain wamefanya maandamano makubwa katika miji kadhaa ya nchi hiyo kupinga waziri wa mambo ya nje wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kukanyaga ardhi ya nchi yao na kuanzishwa uhusiano wa kawaida na Tel Aviv.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa,sambamba na waziri wa mambo ya nje wa Israel Yair Lapid kuwasili nchini Bahrain, wananchi wameandamana katika miji mbalimbali kupinga safari ya waziri huyo wa utawala wa Kizayuni katika nchi hiyo.

Mbali na kuchoma moto bendera ya utawala wa Kizayuni na matairi ya magari, waandamanaji hao waliokuwa wamebeba maberamu ya kupinga utawala wa Aal Khalifa walipaza sauti zao pia kutoa nara za kupinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida na Israel huku wakibainisha uungaji mkono wao kwa harakati za ukombozi wa Palestina.

Watumiaji mitandao ya kijamii nchini Bahrain nao pia wameendesha kampeni maalumu ikiwa na hashtagi za kupinga waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni kuingia katika ardhi ya nchi yao. Wabaharain wanasisitiza kuwa hawawezi kuwasaliti Wapalestina ambao ardhi zao zinakoloniwa na utawala ghasibu wa Israel.

Hayo yamejiri, huku ripoti kutoka Bahrain zikieleza kuwa, askari usalama wa utawala wa Aal Khalifa jana Alkhamisi walisambazwa kwenye njia zote zinazoishia uwanja wa ndege wa Manama ili kukabiliana na hatua yoyote iliyohofiwa kuchukuliwa na wapinzani wa utawala huo.

Wakati huohuo, kiongozi wa Waislamu wa Kishia nchini Bahrain Sheikh Isa Qassim amesema kuhusiana na safari ya waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni nchini humo kwamba, kupatana na adui mzayuni ni vita vya kisiasa vya utawala wa Bahrain dhidi ya watu wa nchi hiyo.

Harakati ya Haq na chama cha Kiislamu cha Al Wifaq nchini Bahrain nazo pia zimesema safari ya Lapid mjini Manama ni utoneshaji wa wazi wa hisia za Wabahrain na kitendo cha uhaini.

Mwezi Desemba mwaka 2020 na kwa upatanishi wa aliyekuwa rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump, Bahrain ilisaini mkataba uliopewa jina la Makubaliano ya Abraham, wa kufanya mapatano na utawala ghasibu wa Israel na kuanzisha rasmi mahusiano ya kidiplomasia na Tel Aviv.  Mapatano hayo yanatazamiwa kuwa ni usaliti kwa ukombozi wa ardhi za Palestina zinazokaliw akwa mabavu na utawala haramu wa Israel.

Hata hivyo wananchi wa Bahrain wametangaza mara kadhaa upinzani wao dhidi ya hatua hiyo ya utawala wa Aal Khalifa.

4001469

Kishikizo: bahrain palestina israel
captcha