IQNA

Sauti ya Abdul Basit inawavutia hata wasiokuwa Waislamu

19:41 - December 01, 2021
Habari ID: 3474626
TEHRAN (IQNA) – Mwanae qarii mashuhuri wa Qur’ani kutoka Misri Sheikh Abdul Basit Abdulswamad amesema baba yake alikuwa na sauti ambayo mbali na Waislamu inawavutia pia wasiokuwa Waislamu.

Akizungumza katika mahojiano ya televisheni kwa mnasaba wa kukumbuka kuaga dunia baba yake, Tariq amesema baba yake aliinukia katika mji wa Armant na alihifadhi Qur’ani kikamilifu akiwa na umri wa miaka 10.

Taria amesema baada ya baba yake kujifunza qiraa, alielekea Cairo ambapo kwa mara ya kwanza alisoma Qur’ani katika Msikiti wa Al Sayyeda Zainab ambapo hadhirina walivutiwa sana na qiraa yake kiasi cha kumbeba mabegani. Baadaye Sheikh Abdul-Basit alijiunga na Radio ya Qur’ani Misri kama msomaji. “Baba yangu alikuwa na sauti ya kipekee. Mwenyezi Mungu alimtunuku na kipawa cha kipekee katika qiraa na tajweed na pia sauti nzuri na uwezo wa kushikilia pumzi kwa muda mrefu.”

Watu wanaposikiliza qiraa yake popote pale duniani basi aya za Qur’ani hutulia katika nyoyo zao. “Hata wasiokuwa Waislamu wanavutiwa na qiraa ya baba yangu na hubakia na mtazamo mzuri baada ya kumsikiliza.”

Jumatatu Novemba 30 ilisadifiana na mwaka wa 33 tokea alipoaga dunia Qarii Abdul Basit.

Qiraa ya Sheikh Abdul Basit Abdul Swamad iliwaathiri watu wengi na hata kuwavutia wasiokuwa Waislamu katika dini ya Kiislamu. Watu 6 waliingia katika dini ya Kiislamu baada ya kuathiriwa na kiraa yake mjini Los Angeles huko Marekani. Aidha inadokezwa kuwa nchini Uganda jumla ya watu 92 walisilimu katika majlisi ya kiraa ya msomaji huyo mashuhuri na watu wengine 72 pia walikubali dini tukufu ya Kiislamu katika majlisi nyingine baada ya kuvutiwa mno na usomaji wake.

4017505

captcha