IQNA

Saudia yalaaniwa kwa kuwanyonga wafungwa 81 wakiwemo Mashia

20:25 - March 13, 2022
Habari ID: 3475034
TEHRAN (IQNA)- Hatua ya utawala wa Kifalme wa Saudi Arabia ya kuwanyonga watu 81 wakiwemo vijana 41 wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia imekbiliwa na upinzani mkali na jamii ya kimataifa, makundi na harakati za kisiasa katika nchi za Kiislamu.

Ni baada ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudi Arabia Jumamosi kuwanyonga watu 81 kwa siku moja, na kuendeleza ukiukaji wa haki za binadamu nchini humo.

Miongoni mwa walionyongwa ni vijana 41 Waislamu wa madhehebu ya Shia wa eneo la Qatif huko mashariki mwa Saudi Arabia, na raia saba wa Yemen ambao walikamatwa na kufungwa na serikali ya Riyadh kwa visingizio mbalimbali.

Naibu Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kulaani mauaji ya kinyama dhidi ya makumi ya Waislamu madhehebu nchini Saudi Arabia ameitaka jamii ya kimataifa kuvunja kimya mkabala wa jinai hiyo.

Ali Nikzad amesema Bunge la Iran linalaani vikali mauaji hayo ya kinyama yaliyofanywa na utawala wa Saudia dhidi ya Waislamu wasio na hatia.

Zarah Sultana, mwanachama wa Chama cha Labour kutoka eneo bunge la Coventry nchini Uingereza, amelaani mauaji hayo ya Waislamu 81 aghlabu yao wakiwa wa madhehebu ya Shia nchini Saudi Arabia na kuandika katika mtandao wa Twitter kwamba: "Leo, utawala wa Saudi umewanyonga watu 81, ambayo ni mauaji makubwa zaidi ya halaiki katika historia ya nchi hiyo."

Sultana amekemea safari ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson  huko Saudi Arabia sambamba na mauaji hayo ya kutisha na kusema: "Kama kweli serikali inajali haki za binadamu, inapaswa kukomesha uhusiano wake wa karibu na Wasaudi."

Habari zaidi zinaarifu kuwa, baadhi ya watu walionyongwa hadi kufa na watawala wa Riyadh walikuwa wanachama wa harakati ya Ansarullah ya Yemen.

Kamati ya Mateka wa Kivita wa Yemen imesema kuwa, hatua ya utawala wa Al-Saud kuwanyonga wafungwa wa kivita wa Yemen ni kinyume cha sheria na ukiukaji wa mikataba yote na kwamba utawala huo unapaswa kusubiri matokeo mabaya ya jinai hiyo.

Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu ya Yemen pia imelaani jinai ya serikali ya Saudia ya kuwanyonga makumi ya watu wanaotuhumiwa kuhusika na ugaidi na kutangaza kuwa: "Kunyongwa Waislamu 81 wasio na hatia wakiwemo raia wa Yemen ni ukiukaji wa wazi wa mafundisho ya dini ya Kiislamu na hukumu za uadilifu na kwamba jinai hiyo imefanywa kwa sababu za kisiasa na kimadhehebu.

Chama cha al Haqq cha Yemen kimeituhumu serikali ya Saudia kuwa inatekeleza mipango ya kijasusi ya Marekani na Uingereza ili kuchochea fitna na hitilafu za kimadhehebu na kidini.

Katibu Mkuu wa harakati ya Asaeb Ahl al-Haq nchini Iraq, Qais al-Khazali amesema: "Saudi Arabia imewanyonga kikatili makumi ya watu kwa sababu za chuki za kimadhehebu." 

Wananchi wa mashariki mwa Saudi Arabia wamekuwa wakiandamana mara kwa mara katika miaka ya hivi karibuni wakilalamikia vitendo vya ukandamizaji vya utawala wa Saudia na mauaji ya makumi ya waandamanaji katika miji ya Al-Awamiyah na Qatif, lakini kila mara wamekuwa wakikandamizwa vikali na kuuliwa na vikosi vya Al-Saud.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema kuwa, Saudi Arabia ni miongoni mwa nchi zinazoongoza dunia kwa kunyonga watu na imekuwa ikilaumiwa sana kutokana na rekodi yake mbaya ya kukanyaga haki za binadamu na kuwanyonga wafungwa wa kisiasa, wanaharakati na wapinzani kwa tuhuma zisizo na msingi kama ugaidi na kadhalika.

4042396

captcha