IQNA

Saudia imeazimia kuwanyonga vijana 40 walioshiriki maandamano ya amani

18:21 - June 20, 2021
Habari ID: 3474025
TEHRAN (IQNA)- Wanaharakati wa haki za binadamu wameonya kuwa, utawala wa Aal-Saud unapanga kuwanyonga makumi ya vijana Waislamu wa madhehebu ya Shia mkoani Qatif mashariki mwa Saudi Arabia.

Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Saudi Leaks, zaidi ya vijana 40 wanakodolewa macho na hukumu ya kuuawa kwa kunyonga, kwa kushiriki tu maandamano mwaka 2011 katika mkoa Qatif ambao aghalabu ya wakazi wake ni Waislamu wa madhehebu ya Shia, mashariki mwa Saudi Arabia.

Jumuiya za kimataifa za kutetea haki za binadamu hivi karibuni zililaani vikali kitendo cha Riyadh kutekeleza hukumu ya kifo dhidi ya kijana Mustafa Mustafa al-​Darwish (26).

Maafisa wa Saudia walimbambikizia kijana huyo tuhuma 13, ya chini kabisa ikiwa ni kushiriki katika maandamano ya watu wa Qatif mwaka 2021 dhidi ya utawala wa kifalme. Watawala wa Riyadh walimkamata kijana huyo Mei 2015 akiwa na umri wa miaka 17 pekee.

Saudi Arabia ni miongoni mwa nchi zinazoongoza dunia kwa kunyonga watu na imekuwa ikilaumiwa sana kutokana na rekodi yake mbaya ya kukanyaga haki za binadamu na kuua wanaharakati na wapinzani wa sera na siasa za utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal-Saud.   Maelfu ya wanaharakati, mashekhe na watetezi wa haki za kiraia wanashikiliwa katika korokoro za Saudi Arabia.

Januari 2016   Saudi Arabia ilitekeleze hukumu ya kifo dhidi ya mwanazuoni mashuhuri wa nchi hiyo, Sheikh Nimr Baqir al Nimr, aliyekuwa maarufu kwa kukosoa dhulma na ukandamizaji wa dola. Ukatili huo wa Saudia wakati huo ulikabiliwa na wimbi la laani na lawama za kimataifa linaendelea kurindima dhidi ya ukatili huo. Wakati huo,  iliwanyonga watu 47 akiwemo mwanazuoni na mtetezi wa haki za binadamu Sheikh Baqir al Nimr ambaye alikuwa mwasisi wa kituo cha kidini cha eneo la al Awwamiyyah huko mashariki mwa nchi hiyo.

Sheikh Nimr ambaye alikamatwa na kutiwa jela muda mfupi baada ya kuanza harakati ya wananchi wa Saudi Arabia ya kupinga siasa za kibaguzi za utawala wa kizazi cha Aal Saud hapo mwaka 2011 kwa tuhuma za kuchochea wananchi na kuongoza harakati ya upinzani ya Waislamu wa madhehebu ya Shia, mwaka 2015 alihukumiwa kifo na mahakama ya nchi hiyo inayosimamiwa moja kwa moja na mfalme wa Saudia na hukumu hiyo ikatekelezwa Januari 2 2016.

Zeid Ra'ad Al Hussein Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa wakati huo alitoa taarifa akiitaja hatua ya serikali ya Saudia ya kuwanyonga makumi ya raia akiwemo, Sheikh Nimr, kuwa si ya kisheria na kutangaza kuwa: Kunyongwa kwa watu ambao walinyimwa hata haki ya kuwa na wakili mahakamani na ambao pia hatia yao haijathibitishwa ni kitendo cha kihalifu na jinai na hakiwezi kukubalika. Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alieleza wasiwasi wake kuhusu ongezeko lisilo na kifani la kesi za kunyongwa watu nchini Saudi Arabia na kusema: Riyadh haipasi kuwanyonga raia na wapinzani kwa sababu tu ya kutoa maoni yanayopinga serikali na utawala.

3474988

Kishikizo: saudi arabia ، vijana ، kuwanyonga ، shia ، qatif
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* :