IQNA

Saudia yalaaniwa kwa kumkamata Shekh Hussein al Nimr

16:37 - December 22, 2020
Habari ID: 3473479
TEHRAN (IQNA) - Taasisi mbalimbali za kutetea haki za binadamu zimetoa radiamali kufuatia hatua ya utawala wa Saudi Arabia kumtia mbaroni mwana wa kiume wa Sheikh Nimr Baqir al Nimr.

Maafisa wa utawala wa Aal Saud wamemtia mbaroni Shekh Hussein al Nimr mtoto wa mwanazuoni mtajika wa Waislamu wa Kishia nchini humo katika fremu ya hatua mpya zinazotekelezwa na utawala huo dhidi ya maulamaa wa kidini mashariki mwa nchi hiyo.  

Taasisi za kutetea haki za binadamu zimekutaja kuendelea kutiwa mbaroni wanazuoni katika eneo la al Sharqiya katika maeneo wanapoishi Waislamu wa madhehebu ya Kishia mashariki mwa Saudi Arabia kuwa ni ukiukaji wa wazi wa sheria na ni ubaguzi wa kikoo na kusisitiza kuwa: hatua hizo hazifanani na madai yanayotolewa na watawala wa Saudia ya kuheshimu haki za binadamu, uhuru  na  utekelezaji mageuzi nchini humo.  

Shirika la Haki za Binadamu la Ulaya na Saudia limelaani kamatakamata iliyoratibiwa na utawala wa Aal Saud ya kuwatia mbaroni maulamaa wa kdini huko Qatif na al Ahsaa mashariki mwa nchi hiyo na kueleza kuwa: utawala wa Saudi Arabia unafanya hivyo tangu huko nyuma kwa kutumia visingizio bandia.

Taasisi mbili za kutetea demokrasia na haki za binadamu na Kituo cha Haki za Binadamu cha Al Khalij pia zimelaani mashambulizi makali yanayofanywa na utawala wa Aal Saud katika mikoa ya Qatif na al Ahsaa na pia vitendo visivyoweza kuhalalishwa na vya kinyume cha sheria vya utawala huo unavyowafanyia maulamaa wa kidini katika maeneo hayo bila ya kubainika wazi tuhuma zinazowakabili.  

Sheikh Baqir Nimr alitiwa nguvuni mwezi Julai mwaka 2012 kufuatia maandamano na malalamiko makubwa ya kudai haki na uadilifu ya watu wa eneo la Qatif mashariki mwa Saudi Arabia lenye Waislamu wengi wa madhehebu ya Shia. Tarehe 15 Oktoba mwaka 2015 Sheikh Nimr alihukumiwa kifo kwa kukatwa kichwa kwa panga na kusulubiwa kadamnasi kwa tuhuma ambazo hazikuwa na msingi eti za kuhujumu usalama wa taifa na kupiga vita utawala wa nchi hiyo. Hukumu ya kifo dhidi ya msomi huyo wa Kiislamu na wenzake 46 waliotambulishwa kuwa ni magaidi, ilitekelezwa tarehe 2 Januari 2016 na kulaaniwa na mataifa ya Kiislamu, nchi na jumuiya mbalimbali za kutetea haki za binadamu. Hivi sasa watu wa Qatif, Saudia Arabia na maeneo mengine dunaini wanajiandaa kumkumbuka mwanazuoni huyo aliyeuawa shahidi. 

3942284

captcha