
Grand Ayatullah Safi Golpayegani, Marjaa Taqlid (mwanazuoni mwenye kuigwa) wa Kishia, alifariki Februari Mosi mwaka huu. Alitambulika kuwa mmoja wa wanazuoni wakongwe zaidi na mwanafaqihi wa zama hizi. Jitihada za kuhakikisha mila na desturi zinabakiwa kuwa hai, kumbukumbu nzuri, hima ya kufanya utafiti na kuwa karibu na watu na wanafunzi zilikuwa miongoni mwa sifa zake.
Mwandishi wa IQNA amezungumza na mhadhiri wa seminari ya Kiislamu Ayatollah Mohsen Faqihi kuhusu haiba ya Ayatullah Safi Golpayegani. Haya hapa mahojiano hayo
IQNA: Unatathminije jukumu la hayati Ayatollah Safi Golpayegani katika kuhimiza kufuata dini kwa kutugemea akili na kujiepusha na khurafa.?
Moja ya sifa zake mashuhuri ni kwamba alipinga uenezaji wa dini kwa njia ya simulizi za ndoto, khurafa, na kauli zisizo na uthibitisho. Hakupenda hata kidogo masuala kama haya.
Katika kueneza dini, baadhi ya watu wananukuu miujiza lakini yeye hakuthamini maneno haya. Miujiza inayosimuliwa inaweza isiwe na mizizi yenye nguvu na huwafanya watu wafuate mitazamo hii badala ya mtazamo wa kimantiki wa dini.
Alisema mara kwa mara kwamba ikiwa unataka kujua kwamba yeye ni mtu mwaminifu na mfuasi wa Ahlul-Bayt (AS), zingatia tabia na maadili yake, hasa uhusiano wake na watu. Kadiri mtu anavyokuwa mwaminifu na mwenye shauku katika kuwatumikia wengine na kutatua matatizo ya maskini, ndivyo anavyokuwa bora zaidi.
Kwa maoni yake, kufanya dhikri, kumtukuza na kumuabudu Mwenyezi Mungu niwajibu wa mja wa Mungu, lakini haitoshi. Muumini anatakiwa kuwatumikia wanadamu wenzake, jamaa na walio karibu naye na afikirie kutatua matatizo yao, na kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu, awe mwenye kupigana kwa njia ya Mwenyezi Mungu au Mujahid kwa kujitoleaa maisha na mali yake. Kipengele hiki ni muhimu na kinaweza kuchukuliwa kuwa kigezo cha kupima udini wa watu binafsi.
IQNA - Je, ina maana kwamba kufanya dhikri, kumtukuza na kumuabudu Mwenyezi Mungu havitoshi kumfanya mtu awe ametekeleza wajibu wa Kiislamu bali kuna haja ya kuwahudumia watu, na pia inapaswa kuangalia vitendo na nia ya mwanadamu?
Ndiyo, dini ni pana na hilo ni jambo ambalo alitilia mkazo hasa kutoa huduma kwa watu ilikuwa mojawapo ya vigezo na vipaumbele vyake vikuu. Pengine sababu ya kutilia mkazo mambo ya kijamii ya ibada, kama vile swala ya jamaa, sala ya Ijumaa, kuhudhuria misikiti, kutembelea wagonjwa, na kuhudhuria mazishi ya Waislamu, ni kwamba wanadamu hawafikirii tu juu ya mtu binafsi na jamaa zao, bali wanafikiri kuhusu wengine na matatizo ya umma kwa ujumla.
IQNA: Ni uwanja gani aliobobea zaidi katika maandishi yake?
Alikuwa na kalamu nzuri na yenye mtiririko na aliandika vitabu venye manufaa kama vile "Al-Hajj" katika juzuu tatu, "Sala", "Khums" na "Kauli ya Kanuni". Darsa zake kwa wanafunzi wake wengi pia zimegeuzwa nna kuwa vitabu. Ayatollah Safi Golpayegani alikuwa mwanafaqhi wa ngazi za juu aliyezingatia misingi.