IQNA

Imam Mahdi atauzaja ulimwengu kwa uadilifu, usalama na usawa

21:19 - March 18, 2022
Habari ID: 3475051
TEHRAN (IQNA)-Tuko katika siku ya 15 ya mwezi mtukufu wa Shaaban ambayo ni siku ya kuzaliwa Mtukufu Imam wa Zama, Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu Aharakishe Kudhihiri Kwake).

Katika alfajiri ya siku kama hii yaani mwaka wa 255 Hijiria, Imam alizaliwa katika mji mtakatifu wa Samarra nchini Iraq. Imam Mahdi (af) ni yuleyule Imam Muahidiwa ambaye baada ya kupitisha kipindi kirefu cha kuwa katika ghaiba, atadhihiri kwa amri ya Mwenyezi Mungu na kuujaza ulimwengu kwa uadilifu, usalama na usawa, baada ya kuwa utakuwa umejaa dhulma na uonevu kutoka kwa madhalimu. Salamu na amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu ya Imam Mahdi (af) na pia salamu ziwaendee wale wote wanaomsubiri Imam kwa kutekeleza majukumu wanaoyopaswa kuyatekeleza kabla ya kudhihiri mtukufu huyo. Tunatoa mkono wa pongezi na fanaka kwa Waislamu wote duniani kwa mnasaba huu adhimu wa kuzaliwa mtukufu huyu ambaye ni mbeba bendera ya uadilifu na wokovu kwa wanadamu wote dhidi ya dhulma na uonevu wa madhalimu.
Tokea zama za kale mwanadamu amekuwa na matarajio ya kuishi kwenye mazingira yaliyojaa amani, usalama na uadilifu na yaliyo mbali na kila aina ya ugomvi, mapigano, machafuko na mivutano. Uislamu ambayo ni dini ya mwisho ya mbinguni na iliyokamilika kila upande, inatoa bishara njema ya kumuandalia mwanadamu mazingira hayo. Tunapozingatia historia ya mwanadamu tunatambua kwamba kufr, ujahili, dhulma, ghasia na umasikini ndizo changamoto kuu ambazo zimekuwa zikiikumba jamii ya mwanadamu. Katika upande wa pili msingi wa serikali ya Imam Mahdi (af) utalenga kuvunja na kuondoa kabisa changamoto hizo. Kwa ibara iliyo wazi zaidi ni kuwa mtukufu huyo (af) atakuja kwa lengo la kueneza fikra ya tauhidi, kueneza elimu, kuvunja misingi ya dhulma, kuwaonyesha wanadamu utamu wa uadilifu, kuwaonyesha njia ya salama na hatimaye kuwafikisha kwenye maisha bora yaliyojaa saada ya milele.
Dola moja duniani
Ibada ya Mwenyezi Mungu mmoja na kuepuka mataghuti na madhalimu ni mafundisho ya msingi yaliyotolewa na mitume na manabii kwa waja wote wa Mungu Muumba. Mtume Mtukufu (saw) pia alisisitiza juu ya tauhidi katika mafundisho yake yote na kusema kuwa uzingatiaji wa suala hilo ndio ufunguo wa wokovu na kufanikiwa mwanadamu katika maisha yake ya humu duniani na huko Akhera. Lengo kuu la Imam Mahdi (af) litakuwa ni kuasisi dola moja duniani lililosimama juu ya msingi wa tauhidi. Ili kufikia jamii moja timilifu wanadamu wanapasa kuwa na fikra na itikadi za pamoja. Itikadi pekee ambayo inaweza kuziunganisha jamii zote za wanadamu ni itikadi inayomwamini Mwenyezi Mungu mmoja na kumuweka kwenye muhimili wa maisha ya kila siku. Lengo hilo bila shaka litathibiti kwa uongozi wa Imam Mahdi (af). Kuhusiana na suala hilo Imam, Swadiq (as) anasema: "Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu, wakati Mahdi kutoka kizazi chetu atakapokuja na kueneza mfumo wake, msingi wa utawaka wake utakuwa ni tauhidi na kuondoa shirki pamoja na hitilafu miongoni mwa mataifa na dini na kuzifanya dini zote kuwa moja."
Uongozi wa kimataifa wa Imam Mahdi (af) utadhihiri duniani kwa msingi wa mafundisho ya wahyi na thamani za kidini. Katika serikali yake masuala yote yakiwemo ya utawala, kubuni sheria, uadilifu na ihsani, miamala ya kijamii, usalama na uchumi yote yatatekelezwa kwa msingi wa tauhidi na ibada ya Mwenyezi Mungu mmoja.
Kupambana na ujahili
Muhimili wa pili wa serikali ya Imam Mahdi (af) utakuwa ni kuyapa thamani masuala yanayohusiana na elimu na kupambana na ujahili. Licha ya maendeleo yote yaliyopatikana katika nyanja za elimu lakini tunaweza kusema kuwa elimu hizo bado ni pungufu na zilizo na kasoro nyingi. Tatizo kubwa zaidi linaloonekana katika elimu hizi za kibinadamu ni kutooana kwa elimu hizo na moyo wa ubinadamu. Kwa mujibu wa baadhi ya wasomi wa nchi za Magharibi kama vile Alexis Carrel, licha ya mwanadamu kufikia maendeleo makubwa ya kielimu katika dunia ya leo, lakini bado ameghafilika pakubwa na mahitaji yake ya kiroho. Alexis Carrel anasema licha ya maendeleo yote ya viwanda yaliyofikiwa na mwanadamu lakini bado ataendelea kuhisi kuwa na kasoro madamu maendeleo hayo hayataenda sambamba na mahitaji yake ya kiroho. Mipango ya Imam Mahdi (af) itakuwa ni ya kueneza elimu na kunyanyua ustawi wa kifikra wa mwanadamu. Kwa maana kwamba wakati wanadamu wanapotatua na kukabiliana na changamoto zao kwa pamoja na wakati huohuo kumuepuka taghuti na kumtii Mwenyezi Muungu mmoja tu, ni wazi kuwa ustawi wao wa kifikra utaimarika.
Katika jamii iliyokamilika ya Imam Mahdi (as) utumiaji akili utaenda sambamba na wajibu wa kumwabudu Mwenyezi Mungu, akhlaki na takua. Ni wazi kuwa elimu na teknolojia ambayo ni maendeleo muhimu ya mwanadamu ikiwa yataenda sambamba na akili salama hatuwezi kushuhudia majanga ambayo leo hii yanamkumba mwanadamu katika pembe tofauti za dunia. Katika serikali ya Imam Mahdi (af) maendeleo ya kielimu yatakwenda sambama na ukamilifu wa kiroho ili yasije yakaanguka kwenye mikono ya watu wasiofaa. Ustawi wa akili unaoenda sambamba na maadili bora hujenga jamii ambayo inafaa kuuongoza ulimwengu.
Kupambana na dhulma
Mpango mwingine muhimu wa serikali ya Imam Mahdi (af) utakuwa ni wa kupambana na dhulma na uonevu na kusimamisha uadilifu, Mtume wa Mwenyezi Mungu anasema: "Hata kama ni siku moja tu itakuwa imebaki kabla ya kumalizika dunia, Mwenyezi Mungu atairefusha siku hiyo kiasi cha kumuwezesha mtu kutoka Ahlul Beit wangu ili aje kuijaza dunia kwa uadilifu na usawa kama ambavyo itakuwa imejaa dhulma na uonevu."
Manabii na mawalii wa Mwenyezi Mungu walitumwa kwa lengo la kuja kuujaza ulimwengu kwa uadilifu na usawa. Ni kwa kuenea uadilifu na hisani ndipo jamii huweza kustawi katika mazingira ya upendo, udugu na huruma. Katika jamii ya Imam Mahdi (af), thamani za upendo, ukarimu, ushirikiano na hisani zitaimarika kadiri kwamba wote watakaoishi katika jamii hiyo watakuwa ni kana kwamba ni watu wa familia moja.
Katika serikali ya Imam Mahdi (af), kila mtu atapewa haki yake na kutoruhusiwa kumdhulumu mwenzake. Tawala zote za kidhalimu zitavunjwa na Imam na watu walio wema tu kupewa fursa ya kutawala. Katika mfumo huo wa uadilifu, kila mtu atasimamishwa mbele ya sheria ya uadilifu na wala hakuna watu wala tabaka lolote la kijamii litakalofadhilishwa juu ya jingine isipokuwa kwa vipimo vya sheria.
Hadithi zilizopokelewa zinasema kuwa katika jamii timilifu ya Imam Mahdi (af), masuala yote muhimu yakiwemo ya kielimu, kiuchumi na kiutamaduni yatanawiri. Watu wanaposhirikiana kwa msingi wa uadilifu na hisani, neema zake Mwenyezi Mungu kwa wanadamu huongezeka na matatizo ya kijamii na kiuchumi kupungua.
Utulivi wa kifikra
Lengo jingine muhimu la serikali ya Imam Mahdi (af) litakuwa ni kuleta utulivu wa kifikra na kiroho na usalama katika jamii. Qur'ani Tukufu inatuahidi kwamba kila mumini awe ni mwanaume au mwanamke, atakayefanya wema Mwenyezi Mungu atampa maisha bora, safi na yaliyojaa utulivu. Katika utawala wa Imam Mahdi (af) tutashuhudia watu wakiishi katika msingi wa imani na matendo mema. Katika jamii hiyo maovu yote yakiwemo ya wivu, chuki, ubakhili na fikra finyu yote hayo yatafutwa. Uhusiano mwema uliojaa upendo na huruma utaimarishwa katika jamii hiyo. Ni irada ya Mwenyezi Mungu kuwa siku ikifika jamii zote za mashariki na Magharibi zitaungana na kwa pamoja kuishi katika kivuli cha tauhidi, uadilifu na maendeleo makubwa ya kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa. Kwa hakika hata kufikiria tu juu ya kuwepo kwa jamii kama hii timilifu na iliyokamilika kila upande ni jambo linalomridhisha mwanadamu.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu atubakishe hai sote ili tuweze kuishuhudia siku hii, ambapo Imam Mahdi, mwokozi wa ulimwengu (af) atadhihiri na kuijaza dunia kwa nuru yake ya uadilifu na usawa kupitia uongozi wake bora na usio na kifani. 
https://iqna.ir/en/news/3478224/hope-for-justice-in-end-times-by-believing-in-mahdi
 
 
 
 

Kishikizo: imam mahdi
captcha