IQNA

Mawaidha

Kuanza Uimamu wa Imam Mahdi (AF)

17:54 - September 24, 2023
Habari ID: 3477648
TEHRAN (IQNA)- Tarehe 9 Mfunguo Sita Rabiul Awwal miaka 1185 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Qamaria, baada ya kuuawa shahidi Imam Hassan Askari (AS) kilianza rasmi kipindi cha uongozi wa Imam wa Zama, Imam Mahdi (-Mwenyezi Mungu Aharakishe Kudhihiri Kwake-AF-).

Imam Mahdi , Imamu wa 12 wa Waislamu wa madhehebu ya Shia ni mwana wa Imam Hassan Askari (AS) na miongoni mwa wajukuu wa Bwana wetu Muhammad (SAW).

Imam Mahdi yuko ghaiba kwa amri ya Mwenyezi Mungu (SW) na hadi mwaka 328 Hijria alikuwa akiwasiliana na watu kupitia wawakilishi wake maalumu.

Kipindi hicho kilipewa jina la "Ghaiba Ndogo". Baada ya hapo kilianza kipindi cha Ghaiba Kubwa ambapo Imam wa Zama hakuainisha mwakilishi makhsusi, na mafakihi wenye ujuzi wa dini ya Kiislamu, wachamungu na watambuzi wa masuala ya zama ndio wawakilishi wa mtukufu huyo katika Umma

 Kwa mujibu wa Hadithi tukufu za Mtume Muhammad (saw), Imam Mahdi (AF) atadhihiri tena kwa ajili ya kueneza haki na uadilifu.

Kwa mujibu wa itikadi ya madhehebu ya Kiislamu ya Shia, Imam Mahdi (AF) anaona na kushuhudia moja kwa moja matendo na mambo yote wanayoyafanya waumini na wafiasi wake hadi wakati wa kudhihiri kwake hadharani utakapowadia. Kudhihiri kwa Imam huyo wa mwisho, kunahitajia kupita wakati na kukomaa kwa akili, elimu na akhlaqi (maadili) ya watu na kuwa kwao tayari kwa ajili ya kushirikiana naye wakati muwafaka.

Atawaongoza wanaadamu kwenye njia nyoofu

Imam huyo wa mwisho wa Mwenyezi Mungu atawaongoza wanadamu wote kwenye njia nyoofu kuelekea kwa Muumba wao wakati ambao atapata fursa ya kuunda serikali itakayosimama juu ya misingi ya mafundisho ya Mwenyezi Mungu, kutekeleza uadilifu na kuheshimu sheria, na bila shaka jambo hilo litawezekana tu wakati wanadamu watakapokuwa tayari kukubali na kufuata miongozo ya mbinguni. La sivyo, iwapo mazingira kama hayo hayatakuwepo kwenye jamii na watu kutokuwa tayari kufuata na kutii maamrisho ya Mwenyezi Mungu kupitia Imam Mahdi (AF), kudhihiri kwake miongoni mwa watu wa aina hiyo hakutakuwa na maana wala faida yoyote. Katika maisha yake ya kijamii, mwanadamu anahitajia serikali na mtawala atakayelinda maisha yake na kumfanya apate maendeleo katika nyanja tofauti. Mwanadamu anapasa kuheshimu na kutii amri za watawala ili waweze kubuni jamii bora, salama, yenye utulivu na inayojitenga na kila aina ya dhulma na uonevu. Lakini kwa bahati mbaya hilo halijaweza kuthibiti bali tunayoshuhudia ni kuwa jamii ya mwanadamu inaendelea kukabiliwa kila siku na ongezeko la dhulma na uonevu.

Hali ya sasa

Hivyo katika mazingira ya hivi sasa ambapo jamii imetumbukia kwenye lindi la matatizo ya kisiasa na kiusalama, fitina kuenea kila sehemu, magonjwa sugu na yasiyo na tiba kuikumba jamii na utovu wa nidhamu na maadili kuenea kila upande, mwanadamu kwa dhati yake anahisi na kutarajia kuwadia siku ambayo itatawaliwa na mtawala anayefuata thamani na miongozo ya Mwenyezi Mungu, ambaye ataweza kutekeleza na kueneza uadilifu katika jamii. Matarajio au kusubiri huko ndiyo mazingira yanayofaa kwa ajili ya kukubalika utawala wa ulimwengu wa Imam Mahdi (AF), ambayo yanapasa kuwa katika kila jamii ya mwanadamu.

Ni wazi kuwa tunapasa kuzingatia nukta hii kwamba kusubiri huku hakupasi kuchukuliwa kuwa na maana ya kupuuza mambo na kukaa kimya. Mwanadamu hapasi kuketi pembeni na kutochukua hatua yoyote ya kurekebisha hali ya mambo katika jamii, bali kusubiri kuna maana ya matumaini na matarajio. Matumaini na matarajio katika maisha ya mwanadamu ndilo jambo linaloathiri na kuchochea zaidi harakati na mapambano yake maishani. Roho na msingi wa matarajio hayo ni kuwa na mtazamo mzuri kuhusiana na mustakbali wake ambao Mwenyezi Mungu amembashiria moja kwa moja kupitia Aya na Riwaya nyingi.

Kishikizo: imam mahdi
captcha