IQNA

Qur'ani inasema nini / 3

Ni vipi tuwe na subira au uvumilivu?

20:12 - May 27, 2022
Habari ID: 3475304
TEHRAN (IQNA)- Kuna misukosuko na masaibu yanayomzunguka mtu kutokana na hali mbaya na matukio mbalimbali. Lakini ni vipi tunaweza kukabiliana na masaibu hayo na kurekebisha mitazamo yetu kuhusu nafsi zetu na ulimwengu?

Katika Qur'ani Tukufu sehemu ya aya ya 155 na 156 ya Surah al Baqarah tunasoma hivi: "

"...Na wabashirie wanao subiri; Wale ambao ukiwasibu msiba husema: Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye hakika tutarejea."

وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُمْ مُصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ؛

Aya hii ya Qur’ani inajulikana kuwa ni Aya ya urejeshaji na inatufundisha somo kwamba kamwe tusihuzunike kwa kutoweka neema, kwa sababu zawadi zote hizi ni za Mungu. Siku moja anasamehe na siku inayofuata anaona inafaa na akaichukua kutoka kwetu neema aliyotupa, na yote mawili ni kwa manufaa yetu.

Ukweli kwamba sisi sote tunarudi kwa Mungu baada ya kifo unatukumbusha kwamba ulimwengu sio wa milele na kwamba kupungua au ukosefu neema au kuongezeka haraka neema hayo yote ni mambo ya kupita kwa muda tu katika dunia hii na zote hizi ni njia ambazo tunapitia. Aidha tunapaswa kufahamu kuwa panda shuka hizo ni katika kumjenga na kumkamilisha mwanadamu.

Uzingatiaji wa kanuni hizi mbili za msingi una athari kubwa katika kujenga roho ya ustahimilivu na subira.

Allameh Tabatabai ameandika katika tafsiri yake ya Qur'ani Tukufu ijulikanayo kama Tafsir al-Mizan kuwa: Wakati mtu anapoamini ukweli wa Mwenyezi Mungu na kwamba Yeye  Ana Mamlaka juu ya kila kitu, kamwe hakasiriki juu ya shida au masaibu, kwa sababu hajihesabu kuwa mmiliki wa kitu anachofurahia kupata au kupoteza.

Sheikh Qar'ati  ameandika katika Tafsir Nur: Mwenye subira, badala ya kujiangamiza na kutafuta hifadhi kwa wengine, huelekea tu kwa Mwenyezi Mungu ili apate kinga na hifadhi. Hii ni kwa sababu kwa mtazamo wake, ulimwengu wote ni darasa na uwanja wa majaribio ambao tunapaswa kukua na kustawi. Dunia hii si mahala pa kudumu mileke, na ugumu wake sio ishara ya kukosa huruma Mwenyezi Mungu. Shida tupatazo ni kama joto chini ya miguu ambayo hufanya tusonge mbele haraka ili tufike eneo salama, kwa hivyo uchungu pia una utamu wake. Masaibu ambayo tunapata hupelekea vipaji vyetu kunawiri na hatimaye kupata thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Pia, kumkumbuka Mungu katika masaibu na misiba tunapotamka kuwa, "..Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu,..." husababisha faraja na mafundisho kwa wanadamu, ni usemi wa Imani ya kweli, ni kielelezo cha Muumini kwa wengine.

Bila shaka, nukta hizi hazipingani na jitihada za kibinadamu za kutatua matatizo, lakini badala yake inasisitiza mtazamo wa kibinadamu. Wanadamu wanaweza kukosa subira kutokana na matatizo, pia wanaweza kuwa wastahamilivu wenye shukrani pamoja na subira. Hayo yanaashiria kiwango cha ufahamu wa mwanadamu katika ufahamu wa falsafa ya masaibu au ugumu wa maisha.

Kama vile mtoto asivyoweza kustahamili viungo kama vile pilipili katika chakula, barobaro anaweza kuistahamili naye mtu mzima huwa ni mwenye kununua viungo hivyo vya chakula.

captcha