IQNA

Qur’ani Tukufu Inasemaje/30

Vyakula Halal katika Qur'ani Tukufu

20:47 - October 06, 2022
Habari ID: 3475889
TEHRAN (IQNA) - Kila dini ina vigezo fulani juu ya aina gani ya chakula wafuasi wake wanaweza kula na nini wengine wanapaswa kuepuka.

Aghalabu ya  dini huwa na vikwazo kuhusu vyakula vinavyoweza kuliwa kutokana na masuala ya afya au kwa sababu nyingine.

Aya za Qur’ani Tukufu zimebainisha ni vyakula gani ni Halal (ambavyo Waislamu wanaruhusiwa kula) au Haram (Waislamu hawaruhusiwi kula). Bila shaka, hakuna vikwazo visivyo na msingi.

Kile ambacho Qur’ani Tukufu inasema kuhusu Haram na Halal kina vipengele vya kuvutia sana. Kwa mfano, Mwenyezi Mungu amefanya baadhi ya vyakula kuwa Haramu lakini vyakula hivyo vinaweza kuliwa chini ya hali fulani.

Kwa mujibu wa Tafsiri ya Qur’ani Tukufu ya Nemouneh, kuna masharti yaliyowekwa kuhusu kula chakula ambacho ni haramu: Kwanza, kinaweza tu kuliwa katika hali za dharura na si kwa furaha na pili, kisiliwe zaidi ya inavyohitajika.

Aya ya 173 ya Sura Al-Baqarah inabainisha  ifuatavyo : “ Yeye amekuharimishieni mzoga tu na damu na nyama ya nguruwe na kilicho tajiwa, katika kuchinjwa kwake, jina la asiye kuwa Mwenyezi Mungu. Lakini aliye fikiwa na dharura bila ya kutamani wala kupita kiasi, yeye hana dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.”

Huenda ikafikiriwa kuwa lengo kuu la Aya ni kuharamisha ulaji wa baadhi ya vyakula lakini ingependeza kujua kwamba wakati wa wahyi Aya hii iliona kuwa ni Halali kula vyakula vingi vilivyokuwa vimeharamishwa wakati wa Jahiliya (zama za kabla ya Muhammad (SAW) kuteuliwa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu).

Nukta nyingine ni kwamba Kanuni ya Iztirar (umuhimu, dharura) haihusu vyakula tu. Wakati kuna Iztirar, sheria yoyote inaweza kuathirika. Kwa mfano, mtu anapokuwa mgonjwa, anaweza kusali akiwa amelala, ikiwa daktari anaamuru.

Anachokataza Mwenyezi Mungu sio tu kwa masuala ya kitiba na kiafya kwani wakati mwingine yanahusiana na masuala ya kiitikadi, kielimu na kiakili. Kwa mfano, kula nyama ya wanyama waliochinjwa bila ya kutaja jina la Mwenyezi Mungu ni haramu ili kujibari au kujiweka mbali na Shirki (ushirikina).

Katika Tafsiri yake ya Noor ya Quran, Hujjatul Islam Mohsen Qaraati anaangazia jumbe zifuatazo katika aya hii:

1- Uislamu unatilia mkazo sana suala la ulaji na lishe na kuonya kuhusu vyakula vyenye madhara na Haramu.

2- Ni Mwenyezi Mungu pekee ndiye anayeweza kukataza au kuruhusu mambo si mengine.

3- Kutaja jina la Mwenyezi Mungu wakati wa kuchinja wanyama ni muhimu ili kwamba chochote tunachofanya kisiwe nje ya uwanja wa Tauhidi na hivyo hiyo ni ishara kwamba tunaweza kupigana kwa madhihirisho yote ya Shirki na ibada ya masanamu.

4- Hali ya dharura hubadilisha sheria lakini kwa masharti.

5- Uislamu ni Dini pana isiyo na mwisho na ina suluhisho kwa kila hali. Wajibu wowote unaweza kuondolewa katika hali ya dharura.

6- Watunga sheria (wabunge) wanapaswa kuzingatia uwezekano wa masharti maalum wakati wa kupitisha sheria.

7- Mtu asitumie vibaya sheria kuhusu hali za dharura na kukiwa na dharura inayoruhusu jambo basi asivuke mipaka.

Habari zinazohusiana
captcha