IQNA

Qur'ani Tukufu Inasemaje / 39

Masafa baina ya biashara na riba kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu

17:13 - December 04, 2022
Habari ID: 3476194
TEHRAN (IQNA) – Matokeo ya riba ni kwamba inasababisha watu dhaifu kifedha kupoteza mitaji yao yote na maisha yao kuharibiwa.

Uchunguzi wa kihistoria na kiakiolojia unaonyesha kwamba uvumbuzi na mzunguko wa pesa ulikuwa mwanzo wa tatizo la riba. Riba ina maana ya kutoa pesa au kitu kama mkopo kwa mtu na kumtaka mkopaji alipe zaidi ya alichokopa.

Ingawa mwingiliano sahihi wa kiuchumi katika jamii unaweza kuleta ustawi wa kitamaduni katika jamii, riba ilikuwa mwanzo wa ukosefu wa haki.

Kwa kuzingatia aya za Qur'ani Tukufu na Hadithi, wanazuoni wa Kiislamu wanaona Riba kuwa ni Haram (iliyoharamishwa kidini).

Imesisitizwa katika maandiko ya Kiislamu kwamba sababu ya kuharamishwa huku ni kupiga vita dhulma kwa upande mmoja na kuendeleza matendo mema ya kijamii kama vile kutoa mikopo kwa wale wanaohitaji kwa upande mwingine.

Riba imeelezwa kuwa kitendo kisichofaa katika dini nyingine za Ibrahimu pia lakini baadhi ya wafuasi wa imani hizo wamepuuza mafundisho haya.

Qur'an Tukufu inasema katika aya ya 275 ya Surah Al-Baqarah: " Wale walao riba hawasimami ila kama anavyo simama aliye zugwa na Shet'ani kwa kumgusa. Hayo ni kwa kuwa wamesema: Biashara ni kama riba. Lakini Mwenyezi Mungu ameihalalisha biashara na ameiharimisha riba. Basi aliye fikiwa na mawaidha kutoka kwa Mola wake Mlezi, kisha akajizuia, basi yake ni yaliyo kwisha pita, na mambo yake yako kwa Mwenyezi Mungu. Na wenye kurudia basi hao ndio watu wa Motoni, humo watadumu."

Allamah Tabatabai katika Tafsiri yake ya Al-Mizan wa Qur'ani amejadili swali la riba, ambapo amefafanua sababu ya Mwenyezi Mungu kuiona kuwa ni mbaya na ya kuchukiza.

Allamah Tabatabai anasema ni kwa sababu matokeo ya riba ni kwamba inasababisha watu dhaifu wa kifedha kupoteza mitaji yao yote na maisha yao kuharibiwa.

Kwa mtazamo wa Qur'ani Tukufu, maingiliano ya kibiashara na kifedha ni sawa lakini riba, kama jambo linaloharibu maadili, kisaikolojia na kiuchumi na kikwazo kwa ukuaji wa mwanadamu ni haramu na inachukuliwa kuwa ni kitendo cha vita dhidi ya Mwenyezi Mungu.

Mtazamo wa uchumi wa aghalabu ya nchi za dunia leo ambao msingi wake ni mwingiliano wa riba imepelekea kuvurgika uchumi hasa miongoni mwa watu wa kipato cha chini katika jamii.

Kuongezeka kwa ubaguzi na pengo la kitabaka katika jamii, kudhoofisha utamaduni wa kufanya kazi na na kuvuruga mchakato wa mgawanyo wa haki na uadilifu wa mali au utajiri katika jamii ni miongoni mwa matokeo mabaya ya riba.

Habari zinazohusiana
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha