IQNA

Qur’ani inasema nini / 5

Kukutana na Mwenyezi Mungu; Mwisho wa masaibu ya maisha

21:58 - June 03, 2022
Habari ID: 3475332
TEHRAN (IQNA)- Masaibu mengi ambayo mwanadamu anapata katika maisha ya ulimwengu hatimaye humalizika kwa kurejea kwa Mwenyezi Mungu, na baada ya ugumu mwanadamu hutarajia faraja.

Kuanzia kuzaliwa, wanadamu huwa katika hali ya kukumbwa na anuwai  ya masaibu pamoja na shida na wako katika hatari kila wakati. Mwanadamu hana hiari mwanzoni na mwisho wa maisha yake, yaani wakati wa kuzaliwa na kifo. Lakini baada ya hapo kuwa na hiari ya kujiainishia mustakabali wake.

Katika sehemu ya aya ya 29 ya Sura Kahf ya Qur’ani Tukufu tunasoma hivi kuhusu nukta hii, “Na sema: Hii ni kweli itokayo kwa Mola wako Mlezi. Basi atakaye, aamini. Na atakaye, akatae…”

Hivyo ni wazi kuwa mwanadamu anaweza kuainisha malengo ya maisha yake. Mwanadamu huwa anajaribu kila wakati na kuvumilia kila ugumu kufikia malengo yake. Lakini mwanadamu hana mamlaka zaidi?

Katika aya ya 6 ya Surat al-Inshiqaaq ya Qur’ani Tukufu tunasoma hivi

 Ewe mtu! Hakika wewe unajikusuru kwa juhudi kumwendea Mola wako Mlezi, basi utamkuta.”

Aya hii ya Qur'ani Tukufu inaonyesha muelekeo wa mwanadamu na inamkumbusha kwamba anapata masaibu katika maisha ya ulimwengu lakini hatimaye atakutana na Mwenyezi Mungu. Kwa kweli, Mungu amemhakikishia na amempa mwanadamu dhamana kwamba ingawa anaweza kukata tamaa chini ya mzigo wa shida lakini amembashiria kwamba mwishowe atakutana naye na kwamba chaguo lake maishani litainisha kiwango cha mkutano wa mja na Mola Muumba. " Katika sehemu ya aya ya 7 ya Suuratul Att'alaaq tunasoma hivi  “...Mwenyezi Mungu atajaalia baada ya dhiki faraja.”

Sheikh Muhsin Qara'ati katika Tafsiiri Nur ya Qur’ani Tukufu anasema:

Mwanadamu anaelekea kwa Mwenyezi Mungu. Kama alivyosema katika Qur’ani Tukufu, ".. Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye hakika tutarejea." (Sura Al Baqarah, 156)

Katika mwendo wa kuelekea kwa Mungu, mwanadamu anakabiliwa na masaibu mengi:

Ewe mtu! Hakika wewe unajikusuru kwa juhudi kumwendea Mola wako Mlezi, basi utamkuta. " (Surat al-Inshiqaaq  6)

Mwenyezi  Mungu ameweka sheria za kila wakati katika historia na jamii ambayo kila mtu hutii na hatimaye hawezi kurejea  kwa mwingine isipokuwa kwa Mola Muumba, “…Mola wako Mlezi, basi utamkuta.”

Hivyo mwisho wa harakati za mwanadamu ni kukutana na Mwenyezi Mungu.

Tafsiri ya maana ya mkutano na Mola Muumba, inahusu mkutano katika siku ya qiyama au ufufuo, ambapo mwanadamu atapata thawabu au adhabu kulingana na aliyoyatenda duniani. Kwa hivyo masaibu ya mwanadamu yataendelea hadi siku ya qiyama ambapo baada ya mwisho wa dunia hii mwanadamu mwenye amali njema atakutana kwa furaha na Mola wake na kisha baada ya hapo atakuwa na maisha yaisyo na mateso au masaibu na yaliyojaa furaha.

captcha