IQNA

Qur'ani Tukufu Inasemaje /22

Tukio la Mubahala; Sisitizo la Qur'ani kuhusu Mazungumzo

15:58 - July 25, 2022
Habari ID: 3475540
TEHRAN (IQNA) – Baada ya tukio la Mubahala lililotokea kufuatia msisitizo wa Wakristo wa Najran juu ya wao kuwa kwenye haki, aya za Qur’an ziliteremshwa zinazotaka mazungumzo na kuzingatia mambo nukta za pamoja. Hii inaonyesha kwamba mtazamo wa Qur'an ambao unatilia mkazo mwingiliano na mazungumzo.

Mubahala ni hali ambayo watu wawili au makundi mawili hutafuta laana ya Mwenyezi Mungu dhidi ya upande mwingine ili kuthibitisha uhalali au wao kuwa kwenye haki.

Tukio la Mubahala lilianza pale Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) alipotuma barua kwa Wakristo wa Najran kuwalingania kwenye Uislamu na likaisha baada ya kughairi madai yao na baadhi yao kusilimu.

Ujumbe kutoka kwa Wakristo wa Najran uliojumuisha zaidi ya wanachama wao kumi waandamizi walisafiri kwenda Madina na baada ya pande hizo mbili kusisitiza juu ya kila moja kuwa kwenye haki, iliamuliwa kuwa suala hilo litatuliwe kupitia Mubahala.

Aya ya Mubahala katika Qur'ani Tukufu, (Aya ya 61 ya Sura Al-Imran) inazungumzia tukio hili: “ Watakao kuhoji katika haya baada ya kukufikilia ilimu hii waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wake zetu na wake zenu, na sisi wenyewe na nyinyi wenyewe, kisha tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo.”

Asubuhi ya Siku ya Mubahala, Mtukufu Mtume Muhammad (SAW)) pamoja na binti yake Bibi Fatima Zahra (SA), mkwe wake Imam Ali (AS) na wajukuu zake Imam Hassan (AS) na Imam Hussein (AS) waliondoka Madina. Abu Haritha, mmoja wa wajumbe waandamizi wa ule ujumbe wa Kikristo, alipowaona wale waliokuwa wakifuatana na Mtukufu Mtume (SAW.), alisema: “Naapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba amekaa kama Manabii walivyokuwa wakiketi kwa ajili ya Mubahala”, na akarejea. Akaongeza: “Kama Muhammad (SAW) hakuwa kwenye haki, asingethubutu kuja kwa Mubahala namna hii, na kama Muhammad (SAW) atakutana nasi katika Mubahala, basi hata Mkristo mmoja hatabaki hai kabla ya mwaka huu kuisha."

Kwa mujibu wa mwanachuoni wa chuo kikuu cha Iran, Rasoul Raoulipour, uhakika wa aya za Qur'ani Tukufu hususan aya zinazokuja katika Surah Al-Imran baada ya aya ya Mubahala, unaonyesha kuwa muelekeo mkuu wa Qur'ani si ule wa Mubahala bali ni mwingiliano baina ya pande hizo mbili na mwongozo kwa njia ya ukweli na haki.

Anasema:

"Wakristo wa Najran walipokataa kufanya Mubahala, iliteremka Aya hii: “ Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lilio sawa baina yetu na nyinyi: Ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote; wala tusifanyane sisi kwa sisi kuwa Waola Walezi badala ya Mwenyezi Mungu. Na wakigeuka basi semeni: Shuhudi- eni ya kwamba sisi ni Waislamu.” (Al-Imran, Aya ya 64).

Mtukufu Mtume (SAW) kisha akawaambia kwamba kwa vile sasa hamtaki kufanya Mubahala, hebu tufikie makubaliano kuhusu mambo yetu ya kawaida.

Mubahala haikufanyika na Qur'anI haikusema tufanye Mubahala kila unapojitayarisha. Badala yake, Quran inasema sasa hebu tuzungumze kuhusu misingi ya pamoja.

Profesa Raoulipour anasema, "nadhani katika Bibilia, katika Agano la Kale na Agano Jipya, kuna msingi wa mazungumzo. Wanadamu hupeleka malalamiko yao kwa wajumbe wa Mungu na kuuliza maswali yao kutoka kwao."

Nukta nyingine ni kwamba ndani ya Qur'ani Tukufu na maandiko mengine matukufu tunaona kwamba Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) na Mitume wengine wa Mwenyezi Mungu wanatukanwa na kulaumiwa lakini wanaendeleza mazungumzo na maingiliano. Kimsingi, maandiko matakatifu yamekuja kuunda mawasiliano na mwingiliano. Lengo kuu la manabii na mitume ni upatanisho. Wamekuja kuwaambia wanadamu wasioijua njia kwamba kuna njia iliyonyooka, kuna Mwenyezi Mungu, na mlinzi yuko, hivyo hupaswi kuwa na wasiwasi.

 

Habari zinazohusiana
captcha