IQNA

Waislamu Australia

Mawaziri wawili wa Kwanza Waislamu Australia wanatambua umuhimu wa uteuzi huo

10:49 - June 02, 2022
Habari ID: 3475325
TEHRAN (IQNA)- Bw. Ed Husic na Bi. Anne Aly ambao wamekuwa mawaziri wa kwanza Waislamu katika historia ya Australia, wanatambua umuhimu wa kuteuliwa kwao na wanasisitiza kwamba wanaangazia sasa kutumia majukumu haya kuleta mabadiliko katika maisha ya Waaustralia.

Kuapishwa kwa wawili hao kuliashiria tukio la kihistoria nchini Australia huku Husic na Aly wakiwa washiriki wa kwanza wa imani ya Kiislamu kuingia katika wizara za kitaifa nchini Australia.

Husic ni mwanamume wa kwanza Muislamu kuhudumu katika baraza la mawaziri, na amechukua wadhifa wa Waziri wa Viwanda na Sayansi.

Kwa upande wake, Bi. Aly ni Waziri wa Elimu ya Awali na Waziri wa Vijana.

Akizungumza na SBS News, Husic alisema kuingia kwenye baraza la mawaziri "bila shaka" kulikuja na "uzito wa majukumu" na hivyo analenga kutoa mchango chanya.

"Huu ni wakati muhimu wa kiishara katika kuleta nchi pamoja", amesema na kuongeza kuwa, "tuna kazi kubwa ya kufanya na tunahitaji watu wengi wanaohusika kufanya kazi pamoja kwa njia sawa ili kuboresha ubora wa maisha kwa Waaustralia wote."

Husic aliongeza uteuzi wake na Aly haukuwahusu wao tu, bali "Waaustralia Waislamu sasa wanafahamu kwamba wanaweza kuwa sehemu ya jambo ambalo ni kubwa."

Aidha amesema uteuzi wao unatuma ishara yenye nguvu kwa Waaustralia vijana wa Kiislamu kuhusu kujihusisha katika masuala ya nchi wakijua kuwa milango ikiwa wazi.

Wote wawili waliapishwa katika nyadhifa zao wakati wa hafla katika Ikulu ya Serikali siku ya Jumatano kwa kutumia Qur'ani Tukufu- walipothibitisha kujitolea kwao kwa nyadhifa hizo mpya.

Husic - ambaye anawakilisha kiti cha magharibi cha Sydney cha Chifley - alikuwa Mwislamu wa kwanza kuchaguliwa kuwa mbunge mwaka 2010.

Yeye ni mtoto wa wahamiaji Waislamu wa Bosnia na aliingia katika siasa baada ya kufanya kazi katika sekta za kibinafsi na za umma.

Inasemekana kwamba, licha ya kujivunia imani yake, hakutaka kuonekana kupitia lenzi moja kama mwanasiasa Mwislamu tu.

Naye Bi. Aly - mwanachama wa kiti cha Australia Magharibi cha Cowan - alizaliwa Alexandria, Misri, na kuhamia Australia na familia yake alipokuwa na umri wa miaka miwili.

Alisema alitumai kisa chaka cha maisha kama  binti wa wahamiaji ambaye baba yake alikuwa dereva wa basi kinaweza kuonyesha kwamba mtu yeyote anaweza kufanikiwa kufikia matarajio yake.

"Ni jukumu kubwa kuhakikisha kwamba ninaweza kuwa wa kwanza lakini mimi si wa mwisho na kuhakikisha kuwa sifungi lango nyuma yangu," aliambia shirika la habari la SBS News.

Bi. Aly ana shahada ya uzamili na PhD kutoka Chuo Kikuu cha Edith Cowan, na alishikilia nyadhifa kadhaa za juu ndani ya utumishi wa umma wa Australia Magharibi kabla ya kuingia katika siasa.

Alifanya kazi pia katika Chuo Kikuu cha Curtin na Chuo Kikuu cha Edith Cowan, akilenga kukabiliana na ugaidi na kukabiliana na itikadi kali kali.

Husic alisema Aly na yeye mwenyewe wametumia mitazamo yao ya kipekee bungeni kutetea masuala kama vile kuzungumzia dhidi itikadi kali za mrengo wa kulia kufuatia mauaji ya ya Waislamu mjini Christchurch katika nchi jirani ya New Zealand. Mauaji hayo yalitekelezwa na gaidi ambaye  ni raia wa Australia..

Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese wa chama cha Leba amesifu utofauti wa baraza lake la mawaziri, ambalo ametangaza kuwa lina idadi kubwa ya wanawake huku 19 wakishika nyadhifa za mawaziri au msaidizi.

3479146

captcha