IQNA

Hali nchini Tunisia

Maandamano nchini Tunisia kupinga kura ya maoni ya katiba

10:28 - June 19, 2022
Habari ID: 3475394
TEHRAN (IQNA) - Waandamanaji wa Tunisia waliingia mitaani katika mji mkuu Tunis siku ya Jumamosi kupinga kura ya maoni kuhusu katiba mpya iliyoitishwa na Rais Kais Saied.

Katiba mpya itamuwezesha Rais Saied kujiimarisha zaidi madarakani. Maandamano hayo yaliyoongozwa na Abir Moussi, kiongozi wa Chama Huria cha Katiba, yalionyesha upinzani unaokua dhidi ya Saied tangu alipotwaa mamlaka ya utendaji mwaka jana, na kulivunja bunge na kutawala kwa amri katika hatua ambayo wapinzani waliita mapinduzi.

Maelfu ya watu waliandamana kutoka Medani ya Bab Souika katika mji mkuu kuelekea Medani ya Kasbah wakipeperusha bendera za Tunisia na kuimba kauli mbiu kama vile "Tunataka kurudisha nchi yetu iliyotekwa nyara."

Saied anataka kurekebisha katiba ili kuupa urais mamlaka zaidi, huku hali ya uchumi ikizidi kuwa mbaya na kukiwa na hofu ya mgogoro wa fedha za umma. Rais Saied ananuia kuweka katiba mpya kwenye kura ya maoni mnamo Julai 25.

Wafuasi wake wanasema anasimama kukabiliana na makundi ya wanasiasa mafisadi ambao wameitumbukiza Tunisia katika muongo mmoja wa kupooza kisiasa na kudorora kwa uchumi.

Hata hivyo karibu vyama vyote vya siasa vya Tunisia vimekataa kura ya maoni iliyopendekezwa, pamoja na chama chenye nguvu cha wafanyakazi cha UGTT.

Hayo yanajiri wakati ambao, Wafanyakazi wa kona zote za Tunisia wanaendelea na mgomo wao ulioitishwa na UGITT huku malalamiko yao makubwa yakiwa ni mishahara na makato ya marupurupu yao.

Chama hicho cha wafanyakazi cha Tunisia kiliitisha mgomo wa nchi nzima siku ya Alkhamisi ili kuilalamikia Serikali kwa kukataa kuongeza mishahara yao, bali ongezeko la makato kwenye mishahara na marupurupu yao, mambo ambayo yanayafanya maisha ya wafanyakazi kutowezekana kabisa wakati huu wa kipindi kigumu cha uchumi na mgogoro wa kifedha uliotokana na migogoro ya kisiasa nchini humo.

3479353

captcha