IQNA

Quds Tukufu

Mashirika ya Kiislamu yaonya kuhusu njama ya Israeli ya kupanua Lango la Magharbeh

20:16 - August 02, 2022
Habari ID: 3475566
TEHRAN (IQNA) - Taasisi za Kiislamu mjini Al Quds (Jerusalem) ziliionya utawala wa Kizayuni wa Israel siku ya Jumapili dhidi ya upanuzi wa Lango la Magharbeh ndani ya eneo la Msikiti wa Al-Aqsa.

Pendekezo la upanuzi linalotafakariwa na utawala wa Israel inaonekana ni kuitikia wito wa wenye itikadi kali za mrengo wa kulia miongoni mwa walowezi wa Kizayuni ambao wanakalia ardhi za Palestina kinyume cha sheria.

Taarifa iliyokuwa na onyo hilo ilitiwa saini na Baraza la Wakfu, Masuala ya Kiislamu na Maeneo Matakatifu; Baraza Kuu la Kiislamu; Darul Ifta ya Palestina; Mahakama ya Jaji Mkuu al-Quds; Idara ya Wakfu ya Kiislamu; na Idara ya Masuala ya Msikiti wa Al-Aqsa

"Miito ya kichochezi inayoendelea inayotolewa na wanaoitwa vikundi vya Temple Mount kupanua lango la Magharbeh ni hatari," yalisisitiza mashirika hayo. "Msikiti na kiwanja chake - yote - ni muhimi katika imani za Kiislamu zinazoshikiliwa na Waislamu kote ulimwenguni."

Vikundi vya walowezi vilipendekeza mpango wa kuondoa kilima cha mchanga na daraja la mbao linalounganisha Lango la Magharbeh na Ukuta wa Al-Buraq, na badala yake kuweka daraja jipya lililopambwa kwa aya za Torati. Aidha wametoa mwito wa uvamizi mkubwa katika Msikiti wa Al-Aqsa mnamo Agosti 9 kuashiria madai ya kuwa eneo hilo lilikuwa na “hekalu lililobomolewa.”

Taasisi za Kiislamu pia zimetahadharisha kuhusu kuongezeka miito, chokochoko na mapendekezo ya Kuyahudisha Msikiti wa Al-Aqswa na kubainisha kwamba, wito na mapendekezo hayo siku zote yanafuatwa na uvamizi mkubwa wa walowezi haramu wa eneo hilo takatifu la Kiislamu. Hakuna sehemu yoyote ya Al-Aqsa iliyo wazi kwa aina yoyote mgao  au ushirikiano wa kiibada baina ya Waislamu na Wakrstio waliongeza, huku wakiusifu usimamizi wa Ufalme wa Jordan katika maeneo matakatifu katika mji  wa Quds unaokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.

/3479929

captcha