IQNA

Kiongozi wa Ansarullah Yemen

Marekani na utawala wa Kizayuni zinaendeleza muelekeo wa maadui wa Imam Hussein (AS)

12:29 - August 09, 2022
Habari ID: 3475598
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen, Sayyid Abdulmalik Badruddin Al-Houthi amesema, Imam Hussein (AS) alisimama kupambana kwa ajili ya kuuokoa Uislamu na shari ya maadui.

Abdulmalik Al-Houthi ameyasema hayo katika hotuba aliyotoa kwa mnasaba wa Siku ya Ashura ambapo sambamba na kukumbusha kuhusu tukio la masaibu makubwa la Karbala ameichambua harakati ya mapambano ya Imam Hussein (AS) kwa kueleza kwamba muelekeo unaofuatwa na Marekani na utawala wa Kizayuni ni mwendelezo wa muelekeo wa maadui wa Imam Hussein (AS).

Kiongozi wa Ansarullah ameongezea kwa kusema: Imam Hussein alikuwa mwendelezaji wa Uislamu wa asili wa Mtume wa Mwenyezi Mungu na alisimama kupambana kwa ajili ya kuuokoa umma wa Kiislamu na Uislamu na shari ya maadui; na mapambano ya Imam Hussein (AS) yalikuwa ni kwa ajili ya kukabiliana na hatua za Bani Umayya dhidi ya dini.

Sayyid Abdulmalik al-Houthi amesema, utawala wa Yazid ulikuwa tishio na hatari kwa umma wa Kiislamu na akaongezea kwa kusema: "sisi ni umma ambao, kama ilivyokuwa zama za Imam Hussein (AS) tunaandamwa pia. Marekani na Israel ni waendelezaji wa muelekeo wa Yazid; na yeyote anayejiunga na safu yao anachukua hatua kwa manufaa na maslahi yao; na hali yake inafanana ya Ibn Ziyad na Shimr.

Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amemalizia kwa kusema: nia ya maadui zetu ni kutaka kutuhodhi na kutufanya watumwa.

3480018

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha