IQNA

Mwezi wa Muharram

Muharram; mwezi wa kukumbuka mapambano ya Imam Hussein AS

21:27 - July 31, 2022
Habari ID: 3475565
TEHRAN (IQNA)- Julai 30, 2022 imesadifiana ni tarehe Mosi Mfunguo Nne Muharram mwaka 1444 Hijria Qamaria. Huu ni mwezi ambao Waislamu na wapenda haki duniani hukumbuka mapambano ya Imam Hussein AS.

Tarehe Mosi Muharram inasadifiana na kuanza mwaka mpya wa Hijria Qamaria. Mwaka wa Hijria Qamaria unahesabiwa kwa mujibu wa mzunguko wa mwezi na katika nchi nyingi za Kiislamu unatumiwa kwa ajili ya masuala ya kidini au hata kijamii. Mwaka wa Hijria Qamaria pia unatumika katika masuala mengi ya kiibada kama vile kuainisha mwanzo wa funga ya mwezi wa Ramadhani, Hija, kuainisha miezi mitakatifu na kwa ajili ya historia ya matukio mbalimbali.

Mwaka wa Hijria ulianzishwa katika zama za utawala wa Khalifa Umar bin Khattab kutokana na ushauri uliotolewa na Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (AS) ambaye aliagiza mwanzo wa hijra ya Mtume kutoka Makka na kwenda Madina uwe mwanzo wa mwaka wa Kiislamu. 

Kabla ya kalenda ya Miladia kutumika kote duniani, nchi nyingi za Kiislamu zilikuwa zikitumia kalenda ya Hijria Qamaria. 

Muharram ni mwezi ambao unahuisha na kurejesha akilini kumbukumbu ya mapambano adhimu na yenye adhama. Muharram ni mwezi uliofungamana na jina la Hussein Ibn Ali (AS) na harakati isiyo na mbadala ya mtukufu huyo katika ardhi ya Karbala. Kila mwaka wakati unapowadia mwezi wa Muharram joto la muunguliko na msisimko huvukuta ndani ya nyoyo na roho za wapenzi wa Bwana Mtume SAW na Ahlu Bayt zake (AS); lakini mwaka huu mwezi wa Muharram na maadhimisho ya mapambano ya Imam Hussein (AS) yameanza katika hali ambayo Waislamu duniani, mbali na kumuomboleza mtukufu huyo, wana majonzi na huzuni pia ya tukio chungu la Mina lililotokea karibuni katika ibada ya Hija.

Hamasa yenye adhama

Tukio ambalo lilisababisha maelfu ya wafanya ziara madhulumu wa Nyumba ya Allah wapoteze maisha katika hali ya kiu na kuziungulisha na kuzitia majonzi nyoyo za Waislamu duniani.

Tukiwa tunaadhimisha hamasa yenye adhama ya Imam Hussein (AS), tunamwomba Mwenyezi Mungu awape daraja tukufu na ya juu mahujaji walioaga dunia huko Mina na azipe subira pia familia na wapendwa wao.

Hamasa ya Imam Hussein (AS) katika ardhi ya Karbala mnamo mwaka 61 Hijria ni mojawapo ya matukio ambayo hayakuishia kwenye mipaka ya mahala na zama. Harakati hiyo adhimu na yenye adhama ilivuka mipaka ya historia na jiografia na kuacha taathira katika zama zote. Kiasi kwamba ujumbe wa mapambano ya Imam Hussein (AS) ungali unazisisimua nyoyo za watu wengi na kuzitia hamasa ya kupambana na dhulma na uonevu. Ni kwa sababu hiyo mapambano ya Imam Hussein (AS) yana umuhimu mkubwa mno katika historia ya Uislamu na hata ya ulimwengu kwa ujumla.

 

Kama mjuavyo, katika zama zote za historia, manabii na mawalii wa Allah, walivumilia tabu na mashaka mengi katika kusimamisha dini ya Allah, kupambana na dhulma na ufisadi na kufanya juhudi kwa ajili ya ukombozi na saada ya wanadamu. Kilichoifanya harakati yao iwe na utakatifu ilikuwa ni nia safi ya kuyafanya hayo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Harakati ya Imam Hussein (AS) nayo pia ilithibiti kwa sababu ilikuwa ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Sababu kuu ya Imam Hussein kuanzisha harakati

Kwa mtazamo wa jumla tunaweza kusema kuwa sababu kuu iliyomfanya Imam aanzishe harakati lilikuwa ni lengo aali na tukufu la harakati hiyo ambalo ni kuhuisha dini ya Allah. Hakuna shaka yoyote kuwa Uislamu umesimama kwa kazi kubwa iliyofanywa na Bwana Mtume SAW na Ahlu Bayt zake, ambao katika vipindi tofauti walijitahidi kuondoa vumbi la bid'a na khurafa lililotanda kwenye sura safi ya dini hiyo tukufu. Matukio mbalimbali yaliyojiri baada ya Bwana Mtume kurejea kwa Mola wake yalithibitisha kuwa baadhi ya watu walifanya juu chini ili kufufua mila na itikadi za zama za ujahilia; na baadhi ya wengine waliokuwa na imani dhaifu waliungana na watu hao na wengine walioamua kunyamaza kimya waliuridhia na kuuidhinisha mpango huo.

Mageuzi yaliyoletwa na Mtume SAW

Kama mnavyojua wapenzi wasikilizaji, kutokana na wito wake wa milele aliokuja nao na shakhsia yake adhimu ya kimaanawi, Bwana Mtume SAW alileta mageuzi makubwa na ya msingi katika jamii ya wakati wake; lakini baada ya kuaga dunia mtukufu huyo harakati ya kurejea kwenye mila na desturi za kijahilia ilipamba moto na kutoa fursa ya kuingizwa bid'a mbalimbali ndani ya dini. Bila ya shaka baada ya kila mageuzi makubwa na mapinduzi, athari za itikadi na mila zilizokuwepo hapo kabla huendelea kubaki na kuwepo uwezekano wa kuirejesha jamii kwenye mila na desturi hizo.
Baada ya Bani Umayya kuhodhi hatamu za mamlaka ya Ulimwengu wa Kiislamu, harakati hiyo iliyojivika vazi la unafiki iliipotosha na kuiondoa kwa kasi kubwa jamii ya Kiislamu kwenye misingi ya mafundisho asili ya Uislamu. Katika mazingira hayo, baadhi ya itikadi na hulka za zama za ujahilia ambazo Bwana Mtume alifanya kazi kubwa ya kupambana nazo zilifufuliwa tena. Suala hili lilifikia kilele mwishoni mwa utawala wa Muawiya na katika zama alipotawala mwanawe, Yazid.

 

Kupotoshwa Uislamu


Baada ya kufa Muawiya, madaraka yalishikwa na mwanawe Yazid. Japokuwa katika hati ya suluhu aliyoandikiana na Imam Hassan (AS), Muawiya aliahidi kuwa hatomtambulisha mtu wa kushika ukhalifa baada yake, lakini kwa kuyakiuka makubaliano hayo alimwezesha mwanawe Yazid kutwaa madaraka. Ili aweze kuendelea kushikilia hatamu za utawala, Yazid alikuwa tayari kupuuza au kupotosha misingi na hukumu za wazi kabisa za mafundisho ya Uislamu. Yazid alikuwa mtu asiyefaa hata chembe kuwa khalifa wa Waislamu, na alionyesha waziwazi jinsi asivyoheshimu na anavyopuuza kutekeleza mafundisho ya dini. Imam Hussein (AS) alikuwa akiuelewa fika ukweli kwamba watu madhalimu wamekuwa wakijionesha kuwa watu wa dini ili kuwatawala watu na kutaka kutumia vazi jipya ili kuufufua tena ujahilia wa zama za kabla ya Uislamu. Walihalalisha aliyoyaharamisha Mwenyezi Mungu na kuharamisha aliyoyahalalisha. Kwa sababu hiyo, alipobainisha lengo lake na sababu ya kumpinga Yazid na kusimama kukabiliana naye, Imam Hussein alisema:"Mimi nimetoka kwa lengo la kurekebisha umma wa babu yangu; na ninataka kuamrisha mema na kukataza mabaya na kufuata sira na sunna za babu yangu Mtume wa Mwenyezi Mungu".

Imam Hussein AS hakunyamaza kimya

Imam Hussein (AS) alikuwa akiitakidi kuwa watawala hawakuwa wakifuata njia sahihi. Jamii ambayo ilikuwa ikiongozwa na kiongozi asiye na mfano, yaani Bwana Mtume Muhammad SAW sasa ilishuhudia hatamu zake za uongozi zinashikiliwa na mtu kama Yazid bin Muawiya. Hakuna popote katika mamlaka za utawala wa Kiislamu iliposhuhudiwa athari hata ya harufu ya uadilifu. Katika zama za utawala wa Bani Umayya, ukabila na mafungamano ya asili na rangi ambayo Bwana Mtume aliyapinga vikali, yalifufuliwa tena, na baada ya muda kupita, mila na desturi za ujahilia zikaanza kupenya ndani ya jamii. Ni kwa namna hiyo jamii ya Kiislamu iliachana kwa kasi na mafundisho asili ya dini.
Katika mazingira kama hayo, shakhsia kama Imam Hussein (AS) hakuweza kuinyamazia hali hiyo. Mtukufu huyo alikuwa akijua kwamba kunyamazia kimya siasa za mtu kama Yazid kutapelekea Uislamu kutoweka. Licha ya Yazid kufanya kazi kubwa ili kwa namna yoyote ile aweze kupata bai'a ya Imam Hussein (AS), lakini Imam alikataa katakata kufanya hivyo, na badala yake akaamua kusimama kukabiliana na watawala madhalimu wa Bani Umayya. Katika harakati yake, Imam Hussein aliweka mkazo katika kuuelimisha umma wa watu wa kawaida na shakhsia muhimu wa jamii ya Kiislamu. Katika mbinu zake za mapambano, mtukufu huyo alieneza fikra na moyo wa kutetea izza na heshima na kukataa idhilali na kunyongeshwa na kusisitiza mno kuhusu uhuru na heshima ya mwanadamu.

Kuhuisha Uislamu

Imam Hussein (AS) alikuwa akikumbusha juu ya mambo hayo matukufu katika kila marhala ya harakati yake.

Kwa kushikamana na usuli na misingi hiyo, Imam Hussein (AS) aliweza kuhuisha na kudumisha milele moyo wa hamasa na ghera ndani ya umma wa Kiislamu. Mtukufu huyo alikuwa akiwatanabahisha watu kuwa wasikubali kwa namna yoyote ile kuridhia dhulma za madhalimu, bali wanyenyekee na kuwa tayari kutii amri za Mwenyezi Mungu tu ambazo ndizo zinazodhamini saada na uokovu wa mwanadamu. Kwa harakati yake ya kipekee ya mapambano, Hussein Ibn Ali (AS) alitoa taswira ya hakika ya kuvutia, ya kwamba wakati dhulma, uonevu na maovu yanapoitawala jamii ya mwanadamu, na nuru ya mema na fadhila tukufu ikawa imefifia na kuzimika inabidi mtu asimame imara kwa ajili ya kuhuisha thamani za dini, hata kama italazimu kuitoa mhanga roho yake katika njia hiyo.

Amani ya Allah iwe juu ya Hussein (AS), hakika iliyo hai daima. Amani na rehma za Allah ziwe juu yake yeye, ambaye kwa sababu ya kuhuisha dini ya Allah alijitolea mhanga maisha yake ili bendera ya uongfu ya Uislamu iendelee kupepea milele.

captcha