IQNA

Sala ya Ijumaa Tehran

Nchi za Ulaya zikumbatie fursa iliyopo ya kushirikiana na Iran

20:39 - September 02, 2022
Habari ID: 3475722
TEHRAN (IQNA)- Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyoswaliwa hapa Tehran amegusia mazungumzo ya nyuklia ya JCPOA, na kuziasa nchi za Ulaya kukumbatia fursa iliyopo ya kufidia na kusahihisha makosa yake mkabala wa mapatano hayo ya kimataifa.

Hujjatul Islam Mohammad Javad Haj Ali Akbari, amesema: “Nchi za Ulaya zisikose fursa ya kushirikiana na Iran, kwa sababu watajuta. Sasa ni wakati wa kufidia jinai zilizofanywa dhidi ya taifa la Iran.”

Kwingineko katika hotuba yake, Khatibu wa Sala ya Ijumaa amesema, Arubaini ya Imam Hussein (AS) ndio mkusanyiko mkubwa zaidi wa wanadamu, na ambao ni wa aina yake na usio na mfano wake duniani.

Hujjatul Islam Mohammad Javad Haj Ali Akbari amesema hayo leo katika hotuba zake za Swala ya Ijumaa hapa Tehran amebaini kuwa, matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein (AS) aidha ndiyo matembezi makubwa zaidi duniani.

Haj Ali Akbari ameashiria mjumuiko huo mkubwa zaidi wa watu ulimwenguni wa Arubaini ya Imam Hussein (AS) na kueleza kuwa, Arubaini ni harakati mashuhuri katika utamaduni wa kisiasa wa Iran na dunia.

Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa hapa Tehran ameongeza kuwa, Arubaini ndio harakati kubwa na mashuhuri zaidi dhidi ya ubeberu na uistikbari katika dunia ya leo.

Tarehe 17 Septemba 2022, itakayosadifiana na tarehe 20 Mfunguo Tano Safar 1444 Hijria itakuwa ni Arubaini ya siku aliyouawa shahidi Imam Hussein (AS), Imam wa Tatu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia duniani pamoja na masahaba zake waaminifu katika jangwa la Karbala.

Mamilioni ya wafanyaziara kutoka pembe zote za dunia ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huelekea mji wa Karbala kusini mwa Iraq ili kuhudhuria shughuli ya Arubaini ya Imam Hussein (AS).

4082625

captcha