IQNA

Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran

Marekani imekuwa na nafasi kubwa katika kuchochea mgogoro wa Ukraine na Russia

20:01 - March 04, 2022
Habari ID: 3475003
TEHRAN (IQNA)- Khatibu wa Muda wa Sala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehrah amekosoa vikali mienendo ghalati ya Marekani katika medani ya kimataifa na kusisitiza kuwa, US ni nembo ya ujahili mamboleo.

Hujjatul Islam Haj Ali Akbari ameashiria matukio ya Ukraine na operesheni maalumu ya kijeshi ya Russia ndani ya ardhi ya nchi hiyo ya Ulaya na kueleza kuwa, Marekani imehusika na matukio yanayoendelea kushuhudiwa Ukraine.

Haj Akbari amebainisha kuwa, Marekani imeunda utawala wa kimafia katika nyuga za utamaduni, uchumi, usalama na uzalishaji wa silaha kwa lengo la kuupa nguvu muundo wake wa kitwaghuti.

Hujjatul Islam Haj Ali Akbari ameeleza bayana kuwa, hakuna shaka kuwa utawala wa Washington umekuwa na nafasi kubwa katika kuchochea mgogoro wa Ukraine na Russia.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Khatibu wa Muda wa Sala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo mjini Tehrah amesema, kwa mujibu wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Marekani ni taifa lenye kupenda kubuni migogoro, na ambalo liliasisiwa kutokana na mauaji ya kimbari na jinai dhidi ya binadamu.

Amesema kutokana na msingi huo wa kuundwa Marekani, nchi hiyo ya kibeberu imeendeleza jinai za kutisha dhidi ya watu wa dunia, sanjari na kuchochea moto wa vita katika pembe mbalimbali za dunia.

Ameongeza kuwa, "kila mmoja anafahamu kuwa Marekani ndiye mhusika mkuu wa kuanzisha vita katika eneo, na bila shaka ndiyo iliyochochea vita huko Ukraine."

Khatibu ya Sala ya Ijumaa hapa Tehran amesisitiza kuwa, kuunda magenge ya kigaidi kama ISIS na kutenda jinai za kuogofya katika magereza ya Guantanamo na Abu Ghuraib ni sehemu ndogo ya jinai za kihaini za Marekani na utawala wa Kizayuni kwa walimwengu.

Kadhalika amesema Iran haiungi mkono vita na inaheshimu mamlaka za kujitawala nchi nyingine duniani, na daima Jamhuri ya Kiislamu ipo tayari kushiriki katika michakato ya kutatua mizozo.

 

4040185

captcha