IQNA

Ibada ya Hija

Wananchi wa Iran waadhimisha sikukuu ya Idul Adha

19:28 - July 10, 2022
Habari ID: 3475485
TEHRAN (IQNA)- Wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamejiunga na wenzaoi duniani leo kuadhimisha sikukuu ya Idul Adha sambamba na Mahujaji wanaokamilisha ibada ya Hija katika mji mtakatifu wa Makka.

Tarehe 10 Dhulhija mahujaji waliokwenda Makka kwa ajili ya ibada ya Hija huchinja mnyama na kutoa sadaka wakitekeleza amri ya Mwenyezi Mungu SW na kuhuisha kumbukumbu ya Nabii Ibrahim (as). 

Mwenyezi Mungu SW alijaribu imani na ikhlasi ya Nabii huyo kwa kumwamuru amchinje mtoto wake kipenzi, Ismail (as), naye akatii na kujitayarisha kuitekeleza. Alimlaza chini na kuanza kukata shingo yake lakini kisu kilikataa kuchinja; ndipo Mwenyezi Mungu alipomtumia mnyama wa kuchinja badala ya mwanawe, Ismail. 

Kwa mnasaba huo wa sikukuu ya Idi, mapema leo miji na maeneo mbalimbali ya Iran yalishuhudia mamilioni ya Waislamu wakishiriki katika Swala ya Idi wakimuomba Mwenyezi Mungu SW saada ya dunia na Akhera.

Swala hiyo mjini Tehran ambayo imehudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu na matabaka mbalimbali ya wananchi, imeongozwa na Hujjatul Islam Walmuslimin Muhammad Jawad Haj Ali Akbari ambaye amesisitiza katika hotuba za swala hiyo kwamba sikukuu ya Idul Adh'ha inatuhimiza kufanya wema na ihsani, kuchinja matamanio ya nafsi na kujisabilia kwa ajili ya Mwenyezi Mungu SW. 

Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA) linatoa mkono wa kheri na baraka kwa Waislamu wote hususan wasomaji wa tovuti wetu kwa mnasaba wa maadhimisho ya sikukuu hii kubwa ya Kiislamu. 

captcha