IQNA

Taazia

Mhubiri wa maarufu wa Kiislamu Sheikh Qaradawi afariki

21:54 - September 26, 2022
Habari ID: 3475845
TEHRAN (IQNA) – Mwanazuoni maarufu wa Kiislamu kutoka Misri Sheikh Youssef al-Qaradawi amefariki dunia siku ya Jumatatu.

Haya yametangazwa katika chapisho katika akaunti yake rasmi ya Twitter ifuatavyo: "Amekwenda kwenye rehema za Mwenyezi Mungu. Kwa hakika, Imam Yusuf al-Qaradawi, alijitolea katika maisha yake kufashiri mafundisho Uislamu, na kutetea umma wake.”

Sheikh al-Qaradawi ambaye alikuwa akiishi Doha, nchini Qatar, alikuwa mwenyekiti wa zamani wa Umoja wa Kimataifa wa Wanazuoni wa Kiislamu (IUMS). Pia alijulikana kama kiongozi wa kiroho wa harakati ya Kiislamu wa Ikhwanul Muslimin iliyoanzishwa Misri na kuenea maeneo mengine duniani.

Sheikh al Qaradawi aliyekuwa na umri wa miaka ya 96 alimkosoa sana Rais wa Misri Abdel Fatah al-Sisi wa Misri kutokana na hatua yake ya kumpindua rais wa kwanza  aliyechaguliwa kidemokrasia Misri, Mohamed Morsi, mwaka 2013.

Morsi, aliyenyongwa  na utawala wa al-Sisi, alikuwa mwanachama mwandamizi wa Ikwanul Muslimin na mfuasi wa Sheikh al-Qaradawi.

Al-Qaradawi  alilazimika kuishi  uhamishoni nchini Qatar tangu 2013 na hata alipewa uraia wa nchi hiyo ya Kiarabu katika Ghuba ya Uajemi. Hatua ya Qatar kumuunga mkono Sheikh al-Qaradawi ilipelekea uhusiano wa nchi hiyo na Misri kuzorota kwa muda mrefu.

Aidha al-Qaradawi alihukumiwa kifo bila kuwepo nchini Misri mwaka 2015 kutokana na harakati zake za kuupinga utawala wa al-Sisi. 

Al- Qaradawi aliandika zaidi ya vitabu 120 ambavyo vilihusu mada mbali mbali za kijamii, kisiasa na kiuchumi katika ulimwengu wa Kiislamu.

Mojawapo ya kazi zake maarufu za mapema ilikuwa kitabu cha 1973 cha Fiqh al-Zakat (Sheria ya Zakat). Al-Qaradawi pia alilenga kutafsiri upya sheria za kihistoria za sheria za Kiislamu ili kuwaunganisha vyema Waislamu katika jamii zisizo za Kiislamu.

3480635

Kishikizo: qaradawi ، ikhanul muslimin ، qatar ، iums
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha