IQNA

Hali ya Al Quds na Palestina

Wanazuoni wa Kiislamu wataka Waislamu waulinde Msikiti wa Al Aqsa

15:48 - May 31, 2022
Habari ID: 3475318
TEHRAN (IQNA)- Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Duniani (IUMS) umetoa wito kwa Waislamu duniani kote na viongozi wa mataifa ya Kiislamu kuutetea Msikiti wa Al Aqsa katika mji wa Al Quds (Jerusalem) ambao unakabiliwa na hujuma ya walowezi wa Kizayuni.

Akizungumzia kadhia hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Duniani Sheikh Dkt. Ali Mohyiddeen Al-Qaradagh amelaani vikali hatua za walowezi za hivi majuzi na kuvunjia heshima Msikiti wa Al Aqsa ambao ni Kibla cha kwanza cha Waislamu.

Aliwataka Waislamu na viongozi wa Kiislamu kuulinda Msikiti wa Al-Aqsa dhidi ya uvamizi wa Wazayuni ambao wanakalia Palestina kwa mabavu.

Sheikh Al-Qaradaghi pia amewataka watu mashuhuri duniani na pia mashirika ya kimataifa kuunga mkono haki za Wapalestina, Waislamu na Waarabu katika Msikiti wa Al-Aqsa, Al-Quds na ardhi zote za Palestina.

Aliendelea kusema kwamba yeye anafuatilia matukio ya Al-Quds na majaribio ya wavamizi wa Kizayuni ya kutaka kuutawala kikamilifu mji huo kwa wasiwasi na huzuni.

Siku ya Jumapili, mamia ya walowezi wa Kizayuni walivamia Kiwanja cha Msikiti wa Al-Aqsa huko al-Quds inayokaliwa kwa mabavu chini ya ulinzi wa polisi wa Israel.

Hapo awali, maandamano ya kila mwaka ya Walowezi wa Kizayuni  kupitia Mji Mkongwe wa Al-Quds siku ya Jumapili yalichukuliwa na Wapalestina kuwa ni uchochezi wa wazi.

Takriban Wapalestina 145 walijeruhiwa wakati wa wanajeshi wa Israel na walowezi  wa Kizayuni walipowashambulia Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na utawala dhalimu wa Israel.

Awali maandamano hayo yalipangwa kufanyika Mei 10, lakini makundi ya mrengo wa kulia ya Israel yalisitisha gwaride hilo lililokuwa na utata baada ya polisi kukataa kuidhinisha na Harakati ya Hamas kuonya juu ya madhara yake.

Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unashuhudia kuongezeka kwa machafuko kila mwaka yanayochochewa na kile kinachoitwa "Maandamano ya Bendera," ambayo ni alama ya kuanza utawala wa haramu wa Israel kukalia kwa mabavu  Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Al Quds Mashariki mwaka 1967.

4060889

captcha