IQNA

Jinai za Israel

Hamas yalaani hatua ya Israel kuwazuia Waislamu kuingia Msikiti wa Ibrahim

18:09 - October 13, 2022
Habari ID: 3475925
TEHRAN (IQNA) - Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imelaani uamuzi wa utawala ghasibu wa Israel kuwazuia Waislamu kuingia katika Msikiti wa Nabii Ibrahim (AS) katika mji unaokaliwa kwa mabavu wa Al Khali (Hebron) katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Katika taarifa yake, Hamas imelaani kuruhusu walowezi wa kikoloni kuunajisi  msikiti huo na kukiuka utakatifu wake kwa kufanya mikusanyiko ya Kiyahudi ndani yake. Aidha Hamas imesema kwamba "vitendo hivyo ni ukiukaji wa wazi wa uhuru wa kuabudu."

"Tunasisitiza kuwa Msikiti wa Ibrahimi ni mahali pa ibada kwa Waislamu pekee, na ukweli huu ulithibitishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) mwaka 2017, na walowezi wa kikoloni hawana haki nayo."

Katika taarifa hiyo, Hamas imewataka wananchi na makundi ya Palestina "kuendelea kupinga ukiukaji wa vikosi vya utawala vya Kizayuni na walowezi wa Kiyahudi wenye itikadi kali."

"Tunatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa na mashirika ya haki za binadamu kulaani na kuharamisha ukiukaji wa Israel na kuunga mkono watu wetu, ardhi na maeneo matakatifu ya Kiislamu na Kikristo."

Katika kikao chake cha 200 mnamo Oktoba mwaka 2016, Baraza la Utendaji la Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) lilipitisha azimio linaloeleza kuwa maeneo mawili ya Haram ya Nabii Ibrahim AS katika mji wa Al-Khalil (Hebron) na msikiti wa Bilal Ibn Rabah huko Bait- Lahm (Bethlehem) ni sehemu zisizotenganishika na ardhi ya Palestina na hazina uhusiano wowote wa kihistoria, kidini na kiutamaduni na Mayahudi.

Kufuatia kupitishiwa azimio hilo na UNESCO, Utawala wa Kizayuni wa Israel uliamua kusitisha ushirikiano wake na shirika hilo la Umoja wa Mataifa.

3480834

captcha