IQNA

Utawala wa Kizayuni wafunga Msikiti wa Nabii Ibrahim AS

12:46 - September 22, 2021
Habari ID: 3474325
TEHRAN (IQNA)- Utawala wa Kizayuni wa Israel umefunga Msikiti wa Nabii Ibrahim AS katika mji wa Al Khalil (Hebron) ulio katika eneo Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, linalokaliwa kabavu na utawala huo ghasibu, kwa lengo la kutekeleza hafla ya Kizayuni-Kiyahudi katika eneo hilo.

Mkurugenzi wa msikiti huo Sheikh Hefzy Abu Sneina amesema maafisa wa utawala wa Kizayuni wameufunga msikiti huo kwa muda wa siku mbili kuanzia Jumanne kwa lengo la kuandaa hafla ya Kizayuni-Kiyahudi.

Imedokezwa kuwa baada ya msikiti huo kufungwa, Wazayuni wameondoa mikeka na mazulia ndani ya msikiti huo na kuwaruhusu Walowezi wa Kizayuni kuingia katika eneo hilo la ibada la Waislamu.

Abu Sneina ameongeza kuwa, tokea mwezi Septemba mwaka huu, wanajeshi wa utawala dhalimu wa Israel wamezuia adhana katika Msikiti wa Nabii Ibrahim AS zaidi ya mara 60.

Walowezi wa Kizayuni wamekuwa wakisherehekea minasaba kadhaa y Kizayuni-Kiyahudi katika mwezi huu wa Septemba na hivyo wametumia fursa hiyo kuzuia adhana katika msikiti huo mtakatifu.

Msikiti wa Ibrahim AS ambao pia ni Haram Takatifu uko katika kitongoji cha kale cha Al Khalil (Hebron) kusini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Kwa mujibu wa baadhi ya Hadithi, ndani ya msikiti huo kuna kaburi la Nabii Ibrahim AS na mkewe Sarah na vile vile makaburi ya Manabii Is-haq na Yaaqub AS na ya wake zao.

Itakumbukuwa kuwa mnamo mwezi Julai mwaka 2017, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) lilitangaza kuwa mji wa Al Khalil ulioko Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan ambao ni moja ya turathi za kimataifa unakabiliwa na hatari kutokana na sera haribifu za utawala wa Kizayuni. 

3999297

 
 
Kishikizo: ibrahimi ، hebron ، al khalil ، palestina ، wazayuni ، walowezi
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha