IQNA

Qur'ani Tukufu Inasemaje /32

Aya kamili zaidi ya Qur'ani Tukufu

16:57 - November 02, 2022
Habari ID: 3476022
TEHRAN (IQNA) – Kuna aya ndani ya Qur’ani Tukufu ambayo inatanguliza sifa 15 nzuri katika nyanja za imani, amali au matendo na maadili na inarejelea itikadi muhimu na kanuni za kivitendo za maadili.

Ni aya ya 177 ya Surah Al-Baqarah: “Sio wema kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi. Bali wema ni wa anaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii, na anawapa mali, kwa kupenda kwake, jamaa na mayatima na masikini na wasafiri, na waombao, na katika ugombozi, na akawa anashika Sala, na akatoa Zaka, na wanao timiza ahadi yao wanapo ahidi, na wanao vumilia katika shida na dhara na wakati wa vita; hao ndio walio sadikisha, na hao ndio wajilindao.”

Aya hii inachukuliwa kuwa ni yenye maelezo mengi zaidi ya Kitabu kitukufu na Mtukufu Mtume (SAW) amenukuliwa akisema kwamba yeyote anayetekeleza mafundisho yake, imani yake itakuwa kamili.

Kuhusu imani, inahusu kumwamini Mwenyezi Mungu, Malaika, Mitume wa Mwenyezi Mungu na vitabu vya Mwenyezi Mungu na katika uwanja wa amali, inazungumza juu ya ibada kama vile sala, masuala ya kiuchumi kama Zakat, masuala ya kijamii kama vile kuwaachili huru watumwa, masuala ya kijeshi kama vile kuwa na subira katika vita, na masuala ya kisaikolojia kama vile subira na ujasiri katika uso wa matatizo.

Katika uga wa maadili, inasisitiza kuwa mwaminifu kwa ahadi anazotoa, kuacha kushikamana na masuala ya kidunia na kuonyesha huruma na kuwasaidia maskini.

Imani katika Mwenyezi Mungu inaongoza kwa kunyenyekea kwa ukweli na imani katika Siku ya Ufufuo huleta hali ya juu na kufuata malengo ya juu. Imani juu ya uwepo wa malaika ni ishara ya kuamini mambo yasiyo ya kawaida. Na imani kwa Mitume ni kuamini mkondo wa uongofu katika historia yote na sababu inayothibitisha kwamba mwanadamu hajaachwa katika dunia hii bila ya mpango na lengo.

Infaq (sadaka, kutoa sadaka) huashiria roho ya ushirikiano na kutoa misaada, sala ni kiungo cha moja kwa moja na Mwenyezi Mungu, Zakat ni kupanga na kutenda kuwasaidia wahitaji, na kutimiza ahadi kunasaidia kuimarisha mahusiano.

Kuhusu Sabr (subira), inasaidia kumfanya mtu kuwa shujaa zaidi. Sabr inaitwa mama wa fadhila zote na Qur'ani Tukufu inaitaja kuwa ni njia ya peponi. Wale ambao wana Sabr katika dunia hii wamepewa hadhi ya juu peponi na Malaika wanawasalimia. “(Wakiwaambia) Assalamu Alaikum! Amani iwe juu yenu, kwa sababu ya mlivyo subiri! Basi ni mema mno malipo ya Nyumba ya Akhera." (Surah Ar-Raad, Aya ya 24)

Qur'ani Tukufu pia inasema kuhusu viongozi wanaofuata kikamilifu mafundisho ya  Mwenyezi Mungu: “Na tukawafanya miongoni mwao waongozi wanao ongoa watu kwa amri yetu, walipo subiri na wakawa na yakini na Ishara zetu." (Surah As-Sajdah, Aya ya 24)

Kuhusu Infaq, ni sharti la kufikia Taqwa kamili (kumcha Mungu, uchamungu). "Na ambao katika mali yao iko haki maalumu, wa mwenye kuomba na anaye jizuilia kuomba." (Sura Al-Maarij, Aya ya 24-25)

Vile vile tunasoma katika Hadithi kwamba kuna sehemu ya mali ya tajiri ambayo ni ya masikini na kwamba mwenye kulala tumbo akiwa ameshiba huku jirani yake akiwa na njaa hana imani kamili kwa Mungu na Siku ya Kiyama.

Baadhi ya jumbe za Aya ya 177 ya Surah Al-Baqarah kwa mujibu wa Tafsiri ya Noor ya Quran Tukufu:

1- Yatupasa kuzingatia madhumini ya dini na si mambo ya kidhahiri na pia tujitahidi kutokengeushwa kutoka katika njia ya malengo makuu.

2- Moja ya malengo ya  Mitume na vitabu vya Mwenyezi Mungu ni kubadilisha tamaduni za watu.

3- Imani inatangulia amali.

4- Uhusiano na Mwenyezi Mungu ni muhimu pamoja na uhusiano na watu na ushirikiano wa kijamii linapokuja suala la matatizo na migogoro.

5- Matendo mema hutengenezwa chini ya mwamvuli wa imani.

6- Katika Uislamu makusudio ya Infaq sio tu kuwasaidia wenye njaa bali pia kumsaidia mwenye kutoa sadaka ili kupunguza kushikamana na mambo ya kidunia.

7- Wachamungu hutoa Zaka katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa kupenda na kwa hamu.

8- Katika Infaq, kuwasaidia jamaa wanaohitaji ni muhimu kuliko kuwasaidia masikini wengine.

9- Dalili ya ikhlasi katika imani ni kutekeleza wajibu wa kidini na wajibu wa kijamii.

10- Mtu ana Taqwa ambaye matendo yake yanathibitisha imani yake.

captcha