IQNA

Jinai nchini Bahrain

Al-Wefaq: Utawala wa Al Khalifah unatumia ziara Papa kuficha jinai Bahrain

5:56 - November 05, 2022
Habari ID: 3476036
TEHRAN (IQNA) - Jumuiya ya Kitaifa ya Kiislamu ya Al-Wefaq ambayo ni kundi kuu la upinzani nchini Bahrain linasema utawala wa ukoo wa Aal Khalifah unatumia vibaya ziara ya Papa Francis nchini humo ili kuficha jinai zake na ukiukaji wa haki za binadamu.

Al-Wefaq imeandika katika taarifa yake iliyochapishwa kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba mamlaka ya Bahrain inakusudia kuchukua fursa ya safari hiyo kwa maslahi yake, licha ya kwamba hali ya haki za binadamu, uhuru wa kujieleza na uvumilivu wa kisiasa nchini humo ni ya kutisha na ni mbaya sana.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, utawala wa Manama unataka kuficha ukubwa wa dhulma na ubaguzi wake wa kimadhehebu, na hayo yanajiri katika hali ambayo, jela na vituo vya wafungwa kote Bahrain vimejaa wanazuoni, maprofesa, wasomi na shakhsia wa kitaifa wanaokabiliwa na mateso na udhalilishaji wa aina zote.

Ikiashiria jinsi watawala wa Bahrain wanavyomfanyia ukatili kiongozi mashuhuri wa madhehebu ya Shia nchini humo Ayatullah Sheikh Isa Qassim,  Al Wefaq imesisitiza kuwa makumi ya wanazuoni akiwemo kiongozi mkuu wa upinzani Sheikh Ali Salman hivi sasa wanashikiliwa korokoroni na mamia ya wengine ni wahanga wa ubaguzi wa kisiasa, kidini, kiutamaduni, kijamii, kiuchumi na kiusalama.

Harakati hii ya upinzani pia imesisitiza kuwa utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifah unakiuka waziwazi haki za binadamu na uhuru wa kiraia, unazuia uhuru wa maoni, dini na imani, unakataa kabisa mazungumzo yoyote, na haujui mipaka wakati wa kuwaadhibu na kuwafunga wapinzani.

Hapo awali mashirika tisa ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yalimtaka Papa Francis kutoa wito wa kukomeshwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu nchini Bahrain na kukemea dhulma na sera za ukandamizaji za utawala wa Al-Khalifa wakati wa ziara yake nchini humo.

Papa Francis Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani hivi sasa anafanya ziara rasmi nchini Bahrain kufuatia mwaliko wa kanisa humo. Atamaliza safari yake mnamo Novemba 6.

Ameratibiwa kutembelea mji mkuu wa Manama na mji wa Awali katika kikao mazungumzo ya kidini.

Mashirika hayo yamesema katika taarifa ya pamoja kwamba Papa anapaswa kuwataka watawala wa kifalme Bahrain kukomesha ukiukaji wa haki za binadamu katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi.

Maandamano ya kupinga utawala yamekuwa yakifanyika nchini Bahrain mara kwa mara tangu maandamano ya wananchi yalipoanza katikati ya Februari 2011.

Washiriki wanautaka utawala wa Aal Khalifah kuachia madaraka na kuruhusu mfumo wa haki unaowawakilisha wananchi wote wa Bahrain uanzishwe.

Utawala wa kifalme unatumia mkono wa chuma kukandamiza wananchi wanaotetea haki zao za kimsingi.

3481119

captcha