Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel imetangaza katika taarifa yake kwamba, baada ya Papa Francis kukosoa vita katika Ukanda wa Gaza, Adolfo Tito Yllana, balozi wa Vatican, ameitwa na kukabidhiwa malalamiko ya utawala huo kutokana na matamshi yaliyotolewa na Papa. Wizara ya Mambo ya Nje ya utawala wa ghasibu wa Israel, imekosoa matamshi ya Papa, ikiyataja kuwa ni ya kukatisha tamaa na kwamba yako mbali na mazingira halisi ya mapambano dhidi ya ugaidi.
Siku ya Jumamosi, Disemba 21, Papa Francis, kiongozi wa Wakatoliki duniani, kwa mara nyingine tena alilaani mashambulizi ya anga ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza, akiyataja kuwa ni kitendo cha ukatili wa wazi.
Akizungumzia shambulio la anga la Israel lililoua wanafamilia kumi, wakiwemo watoto saba, mnamo Disemba 21, Papa alisema, “Jana, watoto walilipuliwa. Huu ni ukatili; hii sio vita. Nataka kusema hivyo kwa sababu inagusa moyo.” Papa Francis ameitaja hali ya binadamu huko Gaza kuwa ni hatari sana na kutoa wito wa kukomeshwa mauaji ya halaiki na jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo hilo na kusisitiza kuwa: "Usitishaji mapigano lazima uanze na misaada itolewe kwa raia ambao wamechoshwa na njaa na vita huko Gaza."
Matamshi haya ya Papa Francis ni sehemu ya hotuba yake katika mkutano na wajumbe wa Baraza la Mawaziri la Papa kwa ajili ya sherehe za Krismasi. Mwezi uliopita, katika sehemu ya kitabu chake kipya, kiongozi wa Wakatoliki duniani alisema kuwa jamii ya kimataifa inapaswa kuchunguza zaidi kuhusu kile kinachotokea Gaza kwa sababu kina sifa za mauaji ya kimbari. Katikati ya mwezi Novemba mwaka huu, wakati wa hotuba yake muhimu, Papa Francis pia aliitaja hali ya sasa katika Ukanda wa Gaza kuwa ni "mauaji ya kimbari" na kusema kwamba jamii ya kimataifa inapaswa kuchunguza suala hili.
Msimamo huu wa Papa umekabiliwa na majibu makali maafisa wa Israel. Wizara ya Mambo ya Nje ya utawala wa Kizayuni imekosoa hadharani matamshi hayo ya Papa Francis aliyekosoa mashambulizi ya Israel huko Gaza akiyataja kuwa ya kidhalimu, na kumtuhumu kiongozi wa Kanisa Katoliki kuwa ana misimamo ya kindumakuwili na eti anapuuza vitendo vya Hamas.
Inaonekana kuwa, sababu kuu ya hamaki na hasira ya viongozi wa ngazi za juu wa Israel dhidi ya Papa ni misimamo yake inayopinga na kulaani jinai za utawala huo hususan mauaji ya kimbari ya Wapalestina huko Gaza. Kwa sababu, hapana shaka kuwa misimamo ya Papa Francis, kama mamlaka ya juu zaidi ya kidini ya Wakatoliki duniani, kwa hakika itaathiri mitazamo ya idadi kubwa ya Wakristo wanaofuata Ukatoliki katika nchi mbalimbali hasa Ulaya, Afrika, Marekani na Amerika ya Kusini, na kusababisha ongezeko la chuki dhidi ya Israel. Takwimu za Vatican zinaonyesha kuwa, kuna wafuasi bilioni moja na laki mbili wa Kanisa Katoliki duniani, na zaidi ya 40% baina yao wanaishi Amerika ya Kusini. Msimamo wa Papa dhidi ya jinai za Israel bila shaka umeathiri mitazamo na maoni ya nchi zenye Wakatoliki wengi na Wakristo wengine, na hali hiyo imesababisha kuzidi kutengwa utawala katili wa Israel katika ngazi ya kimataifa na kupunguza taathira na ushawishi wake.
Licha ya lawama na ukosoaji wa kimataifa dhidi ya Israel na vitendo vyake vya kihalifu, katika kipindi cha miezi 15 ya vita vya Gaza, utawala huo umekataa kusitisha vita na unaendeleza mauaji ya kimbari ya watu wanaodhulumiwa wa Gaza na kutumia silaha ya njaa kuwatesa watu wa eneo hilo. Marekani ikiwa muungaji mkono mkuu wa utawala huo, na washirika wake wa Ulaya kama Uingereza na Ujerumani, zinaendelea kutoa misaada na himaya ya pande zote za kisiasa na kijeshi kwa Israel na kuikingia kifua mbele ya mashinikizo yote ya jamii ya kimataifa
4256325