IQNA

Kombe la Dunia Qatar

Mashabiki Waislamu watamka Shahada kutuma ujumbe kwa rais Macron wa Ufaransa

22:52 - December 16, 2022
Habari ID: 3476258
TEHRAN (IQNA) - Maelfu ya mashabiki Waislamu waliohudhuria mechi ya Morocco dhidi ya Ufaransa nchini Qatar walikariri tamko la Kiislamu la imani, au shahada, siku ya Jumatano, na kutuma ujumbe kwa Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliyekuwa uwanjani hapo.

"Hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu na Muhammad ni mjumbe wake au Laa ilaha illallah Muhammadyur Rasulullah ilisikika katika uwanja katika mji wa Qatar wa Al Khor, wakati mechi kali ya Kombe la Dunia la FIFA ikiendelea kati ya timu hizo mbili.

Tukio hilo lilitokea mara kadhaa katika kipindi chote cha mechi baada ya wito wa wanaharakati wa  "kutikisa uwanja" kwa kudhihirisha mahaba kwa Mtume Muhammad SAW kutoa ujumbe kwa rais wa Ufaransa aliyehudhuria, Emmanuel Macron.

Macron alikutana na kiongozi au Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani mapema mchana na akasimama kwenye uwanja wa jadi wa Souq Waqif saa chache kabla ya mchezo huo.

Siku ya Jumatatu, mwanaharakati mwenye ushawishi katika mitandao ya kijamii Mahmoud Al Hasanat alitumia Twitter kuwataka mashabiki wa Kiislamu wajiunge na onyesho la mshikamano, akisema: "Ninatarajia kusikia kutoka kwa mashabiki wa Morocco katika mechi ya Ufaransa na Morocco, wakimsalia Mtume, Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na familia yake-SAW- katika uwanja”

Wito wake wa kuchukua hatua uliungwa mkono na Boutaina Azzabi Ezzaouia, mwandishi na mfanyakazi wa zamani wa Mtandao wa Al Jazeera, ambaye alishiriki tweet ya Al Hasanat iliyofutwa sasa.

“Wapendwa Wamorocco wenzangu pazeni sauti zenu kwa kumsalia Mtume Muhammad katika mechi inayokuja dhidi ya Ufaransa. Mwacheni Rais Emmanuel Macron na wapambe wake wajue kwamba haturuhusu mtu yeyote kumtukana Mtume wetu mpendwa,” aliandika kwenye chapisho la Instagram siku ya Jumatatu.

Uislamu nchini Ufaransa

Ufaransa kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na uchunguzi wa kimataifa juu ya hisia za chuki dhidi ya Waarabu na Uislamu miongoni mwa wanasiasa wake na watu mashuhuri wa umma.

Rais wa Ufaransa Macron mwenyewe amedai kuwa Uislamu ni dini iliyo  "katika mgogoro" na amesimamia sheria tata ya "kupinga kujitenga" ya Ufaransa, ambayo makundi ya haki za binadamu yanasema imekuwa ikitumika kuwalenga wachache, hasa Waislamu. Chini ya sheria hiyo, makumi ya misikiti ya Ufaransa imevamiwa na kufungwa.

Macron pia ametetea vikali vikaragosi vya chuki dhidi ya wageni vinavyotolewa na vyombo vya habari vya Ufaransa, akisema Ufaransa "haitaacha katuni".

Kabla ya Kombe la Dunia, Waarabu walikuwa tena walengwa wa vyombo vya habari vya Ufaransa, na ripoti iliyochapishwa na gazeti lenye utata ambalo lililenga Qatar. Watumiaji wa mitandao ya kijamii wamelilaani gazeti la Ufaransa la Le Canard Enchaîné kwa ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya Uislamu baada ya kuchapisha picha inayowaonyesha Waarabu wakiwa na mavazi ya soka kama magaidi.

Picha kama hizo zimeonekana hapo awali katika jarida la kejeli la Ufaransa la Charlie Hebdo, ambalo limemdhihaki Mtume Muhammad SAW, likimuonyesha waziri mweusi wa Ufaransa kama tumbili na kukejeli kifo cha mtoto mchanga wa Syria Aylan Kurdi, miongoni mwa mambo mengine.

Hasira juu ya kulinganisha na ISIS

Mchezo wa Morocco dhidi ya Ufaransa siku ya Jumatano ulikuja huku  timu ya taifa ya nchi hiyo ambayo ni maarufu kama Simba ya Atlas kikabiliwa na chuki dhidi ya Uislamu katika vyombo vya habari vya magharibi.

Mtangazaji wa televisheni ya Ujerumani amezua hasira mtandaoni baada ya kulinganisha timu ya taifa ya Morocco na kundi la kigaidi la ISIS au Daesh.

Mtangazaji wa  Welt alionyesha taswira ya wachezaji watatu wa timu ya taifa baada ya mchezo uliofana wa Kombe la Dunia, ambapo waliinua vidole vyao vya shahada.

Hii ni ishara ya kawaida kwa mabilioni ya Waislamu duniani ambapo wakiinua kidole cha shahada inamaanisha imani ya Tauhidi ya Mungu moja.

Hata hivyo, mtangazaji huyo wa Ujermani alifananisha wachezaji na ISIS, akidai ishara hiyo ilisababisha "ghadhabu". Alidai kuwa kuonyesha kidole cha Shahada, “ni salamu ambayo inatumiwa na ISIS.”

Watumiaji wa mitandao ya kijamii walighadhabishwa na ubaguzi wa rangi uliowalenga Wamorocco.

Madai hayo ya kukasirisha yalitolewa siku chache baada ya gazeti la Die Tageszeitung pia kuwakosoa Wamorocco kwa kubebe bendera ya Palestina kama nembo ya uungaji  mkono wao kwa Palestina. Gazeti hilo la Kijerumani limedai kuwa kupandishwa kwa bendera ya Palestinsa katika Kombe la Dunia ni "uhasama uliopangwa dhidi ya Israeli".

Kombe la Dunia la FIFA la Qatar 2022 limefanyika kwa mara ya kwanza kwa michuano hiyo kufanyika katika taifa la Kiislamu na Kiarabu, huku maelfu ya mashabiki wakitumia fursa hiyo kuonyesha uungaji mkono wao kwa Palestina. Bendera za Palestina zimepandishwa katika maeneo ya mashabiki pamoja na viwanja katika muda wote wa mashindano.

Timu za Waarabu zilizoshiriki michuano hiyo hasa Morocco zimekuwa zikishangilia ushindi wao kwa kupeperusha bendera ya Palestina uwanjani.

Mashabiki waliohudhuria mechi wanasema uandaaji wa kihistoria wa mashindano hayo katika nchi ya Kiislamu na Kiarabu kwa mara ya kwanza umetoa jukwaa la mshikamano wa kweli katika ngazi ya kimataifa.

3481683

captcha