Kwa mujibu wa aya za Qur'ani Tukufu, mwili uliosambaratika na kugeuka udongo utakusanywa Siku ya Kiyama kwa amri ya Mwenyezi Mungu.
Uthibitisho wa ufufuo wa kimwili ni mwingi. Aya za mwisho za Surah Yaseen zinaashiria kwa uwazi ukweli huu: “Anahoji kufufuliwa kwetu, lakini amesahau kuumbwa kwake. Amesema, ‘Na akatupigia mfano, na akasahau kuumbwa kwake, akasema: Ni nani huyo atakaye ihuisha mifupa nayo imekwisha mung´unyika? Sema: Ataihuisha huyo huyo aliye iumba hapo mara ya mwanzo. Na Yeye ni Mjuzi wa kila kuumba.” (Aya 78-79 za Surah Yaseen).
Kilichoonekana kuwa hakiaminiki kwa makafiri na kuwafanya kupinga ufufuo ni jinsi tutakavyohuishwa tena baada ya kufa na vumbi letu kutoweka ardhini.
"Nao husema: Tutapo kwisha potea chini ya ardhi, ni kweli tutarudishwa katika umbo jipya? Bali wao wanakanusha kwamba watakutana na Mola wao Mlezi." (Aya ya 10 ya Surah As-Sajdah)
Na walio kufuru walisema: Je! Tukujuulisheni mtu anaye kuambieni kwamba mtakapo chambuliwa mapande mapande mtakuwa katika umbo jipya? Ama amemzulia Mwenyezi Mungu uwongo, au ana wazimu. Bali wasio amini Akhera wamo adhabuni na upotofu wa mbali kabisa. (Aya ya 7-8 ya Surah Saba)
Kwa hiyo, hoja zilizotajwa katika Qur'ani Tukufu kuhusu ufufuo kwa ujumla ni kuhusu ufufuo wa kimwili.
Zaidi ya hayo, Qur'ani mara kwa mara inabainisha kwamba Siku ya Kiyama watu watatoka makaburini. (Aya ya 51 ya Surah Yaseen na Aya ya 7 ya Surah Al-Qamar)
Hii inaonyesha wazi ufufuo utakuwa wa kimwili.
Na kisha kuna hadithi za Ibrahim (AS) na ndege wanne, hadithi ya Uzair aliyehuishwa baada ya miaka 100 na hadithi ya mtu wa Bani Isra’iI aliyeuawa. Wote huangazia kwa uwazi ufufuo wa kimwili.
Pia kuna maelezo mengi ya baraka za kiroho na kimwili wanazopewa watu peponi zinazoonyesha kwamba ufufuo unafanyika katika mwili na roho.
Kwa hiyo, yeyote ambaye ana ujuzi mdogo wa utamaduni na hoja za Qur'ani hatakataa ufufuo wa kimwili. Kwa maneno mengine, kukataa ufufuo wa kimwili ni kukataa ufufuo kwa ujumla.