IQNA

Waislamu Marekani

Mauaji ya Malcolm X: Shirika Kuu la Kijasusi Marekani, CIA, kufunguliwa mashtaka

21:36 - February 22, 2023
Habari ID: 3476609
TEHRAN (IQNA)- Mabinti wa mwanaharakati wa haki za kiraia Muislamu mweusi, Malcolm X, wamesema wataishtaki polisi ya jiji la New York na Shirika Kuu la Kijasusi Marekani, CIA, na Idara ya Upelelezi ya Marekani, FBI, kwa kuhusika na mauaji ya baba yao, hapo 1965.

Mabinti wa Malcolm X, Elisa na Qubilah Shabazz wametangaza hayo katika siku ya kumbukumbu ya mauaji yake wakisema wataifungulia mashtaki CIA, FBI na Idara ya Polisi ya New York kuhusiana na mauaji ya baba yao.

Elisa Shabazz anasema maafisa wa Marekani walificha ushahidi unaoonyesha kwamba "walipanga njama na kutekeleza mpango wa kumuua" babake.

Amesema kuwa CIA, FBI na Idara ya Polisi ya New York walihusika katika mauaji hayo na kusisitiza kuwa watavifungulia mashtaka vyombo hivyo vya kijasusi.

"Malcolm X" aliyekuwa mwanaharakati wa kiraia aliyepigania haki za watu weusi na Waislamu huko Marekani, aliuawa tarehe 21 Februari, 1965.

Alipata umashuhuri kwa mapambano yake dhidi ya ubaguzi wa rangi na kupigania haki za watu weusi.

Kwa miongo kadhaa sasa kumekuwapo maswali mengi kuhusu wahusika wakuu wa mauaji ya Malcolm X.

Malcolm X aliuawa kwa kupigwa risasi akihutubia mkutano. Alikuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa, Wamarekani weusi ambao wanakandamizwa na kubaguliwa na serikali ya Marekani wanaweza kujipatia uhuru na uadilifu chini ya mwavuli wa utawala wa Kiislamu.

Itikadi na misimamo ya mwanaharakati huyo wa Kiislamu iliwachukiza sana watawala wa Marekani na makundi ya ubaguzi wa rangi nchini humo.

4123527

captcha