IQNA

Mufti wa Oman

Utawa wa Kizayuni wa Israel umeingiwa na hofu na wahka kufuatia mapatano ya Iran na Saudia

23:33 - March 18, 2023
Habari ID: 3476726
TEHRAN(IQNA)- Mufti wa Oman Sheikh Ahmad bin Hamad Al-Khalili amesisitiza haja ya kudumishwa amani na utangamano katika eneo la Ghuba ya Uajemi na kubainisha kwamba, makubaliano na mapatano yaliyofikiwa kati ya Iran na Saudi Arabia yameutia hofu na kiwewe utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.

Kufuatia mazungumzo ya hivi karibuni kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudi Arabia mjini Beijing,China nchi hizo mbili zimekubaliana kurejesha uhusiano wa kidiplomasia baada ya kupita miaka saba.
Kwa mujibu wa ripoti ya tovuti ya Al-Khalij Online Sheikh Al-Khalili amesisitiza kuwa mihimili ya utawala ghasibu na mkaliaji ardhi kwa mabavu wa Kizayuni imetetereka; na Wazayuni wamepatwa na mshtuko ndani ya nyoyo zao baada ya kufikiwa mapatano kati ya Iran na Saudi Arabia.
Sheikh Ahmad bin Hamad Al-Khalili ameongezea kwa kusema: "Utawala wa Kizayuni umefikia yakini kwamba makubaliano kati ya Iran na Saudi Arabia ni kengele ya utawala huo kuondoka milele."

Mufti wa Oman aidha amepongeza nafasi na mchango wa Oman katika kufikiwa makubaliano hayo kati ya Iran na Saudi Arabia na kuzitaka pande zote kuzingatia taqwa na uchamungu na kudumisha suluhu na mwafaka ziliofikia.

Itakumbukwa kuwa mnamo tarehe 3 Januari 2016, Saudi Arabia ilivunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Iran kwa kisingizio cha baadhi ya watu kushambulia ubalozi mkuu na ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Tehran na Mashhad.

4128617

captcha