IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu

Iran yalaani kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Denmark

15:48 - March 29, 2023
Habari ID: 3476779
TEHRAN (IQNA)- Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani wimbi la kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu na makundi yenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia nchini Denmark na katika nchi nyingine za Ulaya.

 Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekosoa vikali wimbi hilo la kuvunjiwa heshima Kitabu Kitukufu cha Waislamu katika nchi kadhaa za Ulaya na kueleza kuwa, vitendo hivyo vinahatarisha amani na kuishi kwa utangamano jamii ya wanadamu.

Kan'ani amekosoa pia kimya cha wale wanaojinadi kuwa watetezi wa haki za binadamu duniani, kwa kufumbia macho vitendo hivyo vya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu. Amesema vitendo hivyo havitakuwa na tija nyingine isipokuwa kuchochea misimamo mikali, ghasia na kuhatarisha usalama wa dunia.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema hayo chini ya wiki moja baada ya kundi lenye chuki dhidi ya Uislamu la Patrioterne Gar Live, kuchoma moto nakala ya Qur'ani huko Copenhagen, mji mkuu wa Denmark.

Aidha mapema mwaka huu, Rasmus Paludan, mwanasiasa mwenye misimamo mikali wa Denmark alichoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu karibu na Ubalozi wa Uturuki mjini Stockholm huku akiwa analindwa na polisi ya Sweden.

Siku chache baadaye, Edwin Wagensveld, mwanasiasa wa siasa kali za mrengo wa kulia wa Uholanzi, na kiongozi wa kundi la chuki dhidi ya Uislamu la Pegida, alirarua kurasa za Qur’ani Tukufu huko The Hague, mji mkuu wa Uholanzi. Video ya Wagensveld kwenye Twitter ilionyesha kuwa alichoma kurasa zilizochanwa za Qur’ani Tukufu.

Vitendo hivi vimelaaniwa vikali na Waislamu pamoja na nchi za Kiislamu duniani ambapo serikali za Sweden na Uholanzi zimekosolewa kwa kuunga mkono vitendo hivyo viovu.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu na nchi nyingine za Kiislamu duniani zinataraji mamlaka za Denmark zitawajibika na kufut kibali cha kuruhusu vitendo hivyo vinavyoumiza hisia za Waislamu na vinavyokolewa moto wa chuki za kidini.

3482969

captcha