IQNA

Jinai za Israel

Israel yashambulia Gaza, Lebanon kufuatia ulipizaji kisasi cha hujuma dhidi ya al-Aqsa

9:50 - April 07, 2023
Habari ID: 3476825
TEHRAN (IQNA)- Jeshi la utawala katili wa Israel lilishambulia maeneo ya Lebanon na Palestina katika Ukanda wa Gaza mapema Ijumaa, kufuatia kuvurumishwa makombora ya kulipiza kisasi kutoka Gaza na Kusini mwa Lebanon kutokana na mashambulizi ya kinyama ya utawala huo dhidi ya waumini wa Kipalestina ndani ya Msikiti wa al-Aqsa katika mji unaokaliwa kwa mabavu wa Quds (Jerusalem).

Ndege za kivita za utawala ghasibu wa Israel zimelenga  eneo la Hay al-Zeitoun kusini mwa Mji wa Gaza kwa makombora matatu, kando na kushambulia maeneo mengine mbalimbali katika eneo hilo ambalo liko chini ya mzingiro wa kinyama wa utawala huo wa Kizayuni.

Punde baada ya mashambulizo hayo ya angani Israel, harakati za mapambano ya Kiislamu Ukanda wa Gaza zilijibu kwa misururu ya roketi.

Katika kulipiza kisasi kufuatia hujuma za Israel dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa, wanamapambano wa Kiislamu walivurumisha makombora katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ambazo zimepachikwa jina la Israel na kupelekea  ving'ora vya hatari kusikika katika mji wa Sderot pamoja na vitongoji haramu vya Nirim na Nir Am karibu na mpaka wa Gaza.

Aidha siku ya Alhamisi, takriban roketi 30 ziliripotiwa kurushwa kutoka kusini mwa Lebanon hadi ndani ya Israel kulipiza kisasi uvamizi wa Israel dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa.

Mapema Ijumaa, jeshi la utawala wa Israel lilisema limeshambulia maeneo ya Hamas kusini mwa Lebanon, ambapo wakaazi karibu na eneo la kambi ya wakimbizi ya Rashidiyeh waliripoti milipuko mitatu mikubwa.

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imeapa kwamba Wapalestina hawatabakia kimya mbele ya vitendo vya uchokozi vinavyoendelea vya utawala ghasibu wa Israel vinavyolenga Msikiti wa al-Aqswa katika mji mtakatifu wa Quds unaokaliwa kwa mabavu.

Kiongozi wa Hamas katika Ukanda wa Gaza Ismail Haniyeh, amesema, "Watu wetu wa Palestina na makundi ya mapambano ya Kiislamu ya Palestina hawatakaa kimya" na watakabiliana na "uchokozi wa kinyama" wa utawala ghasibu wa Israel dhidi ya al-Aqsa.

4132008

Habari zinazohusiana
captcha