Katika uhalifu wao wa karibuni, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wameshambulia raia wa Palestina waliokuwa wakiswali ndani ya Msikiti wa al Aqsa, na wakati huo huo kuwajeruhi na kuwatia nguvuni Wapalestina wengi; vitendo vilivyolaaniwa pakubwa kimataifa.
Msikiti wa al Aqsa ambao ni nembo kuu ya utambulisho wa Kiislamu na Palestina wa mji wa Baitul Muqaddas, mara kwa mara umekuwa ukikabiliwa na hujuma za uvamizi na uharibifu za utawala ghasibu wa Israel unaoikalia Quds Tukufu kwa mabavu.
Muhammad Bagheri Qalibaf, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran amesema leo katika kikao cha wazi cha Bunge kwamba: Kwa kuwepo nguvu ya muqawama, utawala wa Kizayuni unajua kuwa adhabu kali inaungojea katika siku iliyoahidiwa.
Qalibaf amelaani vikali kuvunjiwa heshima Msikiti wa al Aqsa, kibla cha kwanza cha Waislamu, kutiwa nguvuni, kupigwa na kuhujumiwa raia wa Palestina waliokuwa kwenye ibada ya itikafu katika eneo hilo takatifu.
Amelaani pia vikali mashambulizi ya kinyama ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni huko Gaza na kusini mwa Lebanon na kuongeza kuwa: Kwa miongo kadhaa, utawala wa Kizayuni umegeuka na kuwa chombo cha mauaji kisichodhibitiwa na kilichopindukia kwa kufanya uhalifu kupitia kupuuza na kukiuka sheria zote za kimataifa.
4132520