IQNA

Taarifa ya Iran

Kuvunjiwa heshima tena Qur'ani tukufu nchini Denmark ni kuwatusi dhahir shahir Waislamu wote duniani

20:49 - April 16, 2023
Habari ID: 3476875
TEHRAN (IQNA)- Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Nasser Kanani amelaani vikali kitendo cha kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu kilichofanywa nchini Denmark.
Nasser Kanani amesema: "kitendo hiki kiovu, ambacho kimefanywa na kundi lenye itikadi kali na misimamo ya kufurutu mpaka katika mwezi mtukufu wa Ramadhani - mwezi ilioteremshwa Qur'ani, ni dharau kwa dini ya mbinguni na ing'arayo ya Uislamu na ni kuwatusi dhahir shahir Waislamu wote duniani.
 
Kanani amefafanua kuwa: kitendo hiki cha kifidhuli na cha kichochezi kilichofanywa siku ya Ijumaa, wakati watetezi wa uhuru duniani walikuwa wakipaza sauti zao kwa pamoja kutoa wito wa kukombolewa Quds Tukufu kutoka kwenye makucha ya utawala wa fitna na mtenda jinai wa Kizayuni, ni njia ya kipuuzi zaidi ya kudhihirisha madai yanayotajwa katika ulimwengu wa Magharibi kuwa ni uhuru wa kutoa maoni.
 
Msemaji wa vyombo vya kidiplomasia vya Iran amekumbusha kuwa kuyatusi bila kizuizi chochote matukufu ya Waislamu ni upande mwingine wa sarafu ya wenye misimamo kufurutu mpaka na ukatili wa kitakfiri, ambao unastahili pia kulaaniwa na kudhibitiwa kimataifa.

Kanani ameitaka serikali ya Denmark ichukue hatua madhubuti za kuzuia kurudiwa kwa vitendo hivyo vya chuki.

 
Kuvunjiwa heshima tena Qur'ani Tukufu nchini Denmark kumefanyika wakati watu wenye misimamo ya kufurutu mpaka walichukua hatua kama hiyo mnamo tarehe Machi 23 katika mji mkuu wa nchi hiyo Copenhagen.
 
Mnamo Januari 27 pia, mtu mmoja mwenye misimamo ya kufurtu ada  aliichoma moto nakala ya Qur'ani tukufu mbele ya msikiti na karibu na ubalozi wa Uturuki mjini Copenhagen. Mnamo Januari 21, tukio kama hilo lilifanyika huko Stockholm, mji mkuu wa Sweden.
 
Vitendo hivyo viliamsha hasira za nchi za Kiislamu na Waislamu duniani. Waislamu walioandamana kulaani vitendo hivyo walizitaka serikali za Sweden na Denmark zichukue hatua za kuzuia kurudiwa vitendo hivyo, hata hivyo inavyoonekana serikali hizo zimeupuuza wito huo.
3483216
captcha