IQNA

Njama za Mabeberu

Marekani, Uingereza zinazuia mapatano ya amani kati ya Yemen na Saudi Arabia

18:10 - May 02, 2023
Habari ID: 3476947
TEHRAN (IQNA)- Katika hali ambayo, Saudi Arabia na Yemen zimepiga hatua muhimu kwa ajili ya kuhitimisha vita vya Yemen, mashinikizo ya serikali ya Marekani kwa utawala wa Riyadh yamekuwa kikwazo na kizingiti kikuu cha kuhitimishwa vita hivyo.

Katikati ya mwezi uliopita wa Aprili, ujumbe wa Saudi Arabia uliwasili Sana'a mji mkuu wa Yemen. Hiyo ilikuwa safari ya kwanza ya ujumbe wa Saudia huko Yemen tangu kulipoanza vita katika nchi hiyo mwaka 2015. Safari ya ujumbe wa Saudia huko Yemen ilifanyika katika hali ambayo, kabla ya hapo, Riyadh haikuwa tayari hata kufanya mazungumzo na Harakati ya Wananchi ya Ansarullah na serikali ya Yemen yenye makao yake huko Sana'a, seuze ujuumbe wake uelekee Yemen. Hivyo basi, safari ya ujumbe huo ilikuwa na maana kubwa nayo ni Riyadh kuitambua rasmi serikali ya Yemen yenye makao yake katika mji mkuu wa Yemen Sana'a.

Sambamba na safari ya ujumbe wa Saudia, ujumbe kutoka Oman nao ulifanya safari huko Yemen. Kufanyika kwa pamoja safari za jumbe mbili hizo huko Yemen ni ishara ya wazi na bayana ya kuwa na azma ya dhati pande zingine kwa ajili ya kuhitimishwa vita vya Yemen ambavyo vimebomoa na kuharibu sehemu kubwa ya miundomsingi ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu. Hii ni kutokana na kuwa, ujumbe wa Oman unaaminiwa na pande zote mbili za Saudia na Yemen. Dr. Shireen al-Adeimi, mweledi na mchambuuzi wa masuala ya Asia Magharibi ameandika: Safari ya ujumbe wa Saudi Arabia ambayo nukta yake muhimu ya kuanzia ilikuwa ni kupeana mikono Mahdi al-Mashat wa Yemen na Muhammad al-Jaber wa Saudia  ni ishara ya wazi ya kutokea mabadiliko makubwa na ya kuhisika katika vita vya muda mrefu na mzingiro dhidi ya Yemen, vita ambavyo hadi sasa vimesababisha zaidi ya Wayamen 375,000 kuuawa na kuwafanya mamilioni ya wengine kuwa katika hatari ya kufa njaa.

Licha ya kuwa katika hatua ya awali kulifikiwa makubaliano muhimu ambapo kuachiliwa huru mateka kilikuwa moja ya vipengee vya makubaliano hayo kilichofanyiwa kazi, lakini matukio ya baada ya hapo yanaonyesha kuwa, hakujafikiwa makubaliano ya mwisho ya kuhitimisha vita hivyo.

Sababu kuu ya kujitokeza mkwamo wa kufikiwa makubaliano ni ukwazaji mambo wa Marekani pamoja na mashinikizo yake dhidi ya Riyadh. Marekani ambayo imechukizwa mno na hatua ya kufikiwa makubaliano baina ya Saudi Arabia na Iran ya kuhuisha makubaliano ya kidiplomasia baina yao na inaona makubaliano hayo kuwa hayana maslahi na Washington, hivi sasa inaishinikiza Riyadh ili iachane na mchakato wa kufikia makubaliano na Yemen.

Ali al-Qahum, mjumbe wa Idara ya Kisiasa ya Harakati ya Ansarullah ya Yemen sanjari na kusisitiza kwamba, kufanya harakati kuelekea upande wa amani ni msimamo sahihi amesema kuwa: Saudi Arabia inapasa kuondoka chini ya bendera ya Marekani. Saudia lazima ikabiliane na mashinikizo ya madola ya Ulaya ya kuendeleza vita na mzingiro dhidi ya Yemen. Lengo la Wamagharibi ni kuifanya Saudia inase katika kinamasi cha vita vya Yemen na iwe na uadui na majirani zake ambapo baada ya hapo malengo ya kikoloni yatakuwa wazi na bayana.

Muhammad al-Bukhaiti, mjumbe mwandamizi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesisitiza pia katika mahoajino aliyofanyiwa na kanali ya televisheni ya al-Mayadeen kwamba: Marekani na Uingereza hazitaki amani ipatikane nchini Yemen na kila mara tawala hizo zinapohisi kwamba, kumepigwa hatua katika mazungumzo, basi hufanya njama ili hatua hiyo iliyopigwa isizae matunda, na wakati mazungumzo yasipofikia natija basi chaguo la nguvu za kijeshi huwekwa mezani.

Upinzani wa Marekani dhidi ya kufikiwa makubaliano baina ya Saudia na Yemen ya kumalizika vita una sababu nyingi hata hivyo muhimu zaidi ni kwamba, Washington haina hamu kabisa wala shauku ya kuhimitishwa vita hivyo pasi na kushirikishwa yenyewe au vita hivyo vifikie tamati kwa msaada wa mataifa kama China au Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Marekani inaamini kuwa, kufikia tamati vita hivyo katika mazingira ya sasa ni kwa maslahi ya mhimili wa muqawama na eneo la Asia Magharibi na wakati huo huo hilo litakuwa ni kwa madhara kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Ni kwa muktadha huo, ndio maana Marekani imetia vigingi katika njia ya kufikiwa makubaliano baina ya Saudia na Yemen kwa ajili ya kumaliza vita na inaishinikiza Riyadhj ili isititshe mazungumzo yake na Yemen.

3483402

captcha