IQNA

Haki za Binadamu

Ripoti ya Iran kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na tawala za Marekani na Uingereza

18:14 - December 16, 2024
Habari ID: 3479910
IQNA-Kwa mujibu wa ripoti ya kila mwaka ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa Marekani na Uingereza, ripoti ambayo imeandaliwa kwa kutelekeza mswada uliopitishwa na Bunge la Iran mwaka 1391 Hijria Shamsia,

 

Marekani imezipuuza na kuzibeza sheria zote za kimataifa, ripoti, taarifa na misimamo ya taasisi za haki za binadamu na kufuta itibari ya hati na nyaraka zote za kimataifa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Ukiukwaji wa Haki za Binadamu uliofanywa na Marekani mwaka 2024, ni wajibu wa nchi zote huru na zinazojitegemea kuyaweka hadharani matukio ya ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa ndani ya Marekani ili kuwadhihirishia walimwengu namna viongozi wa Marekani wasivyo wakweli katika madai yao ya kuheshimu haki za binadamu na jinsi wasivyozijali sheria za kibinadamu, hali ambayo imewaathiri watu wengi nchini Iran na kwenye nchi nyinginezo.

Ijapokuwa dhana ya haki za binadamu ni kitu kinachokubaliwa na Jamii ya Kimataifa na katika ngazi ya kimataifa, lakini tukiitupia jicho mitazamo, misimamo na matendo ya nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani tutabaini kuwa, Wamagharibi wana tafsiri yao mahususi na yenye mipaka maalumu ya dhana hii ya msingi; na wana vigezo na vipimo maalumu wanavyotumia katika kuchunguza na kuchukua misimamo kuhusiana na hali ya haki za binadamu katika nchi zingine, hususan zile zinazopinga ubeberu wa Magharibi.

Ukweli ni kuwa suala la haki za binadamu lina sura, vigezo na pande kadhaa wa kadhaa katika maeneo tofauti ya dunia, kwenye nchi mbalimbali na katika dini tofauti; na kwa hiyo si sahihi hata kidogo kwamba Magharibi ikae kitako na kutumia tafsiri yake mahususi ya haki za binadamu ili kuzitolea nchi zingine juu ya suala hilo.

Suala la undumakuwili

Suala la undumakuwili unaofanywa na nchi za Magharibi katika uga wa haki za binadamu limeshapigiwa kelele mara nyingi na nchi zinazopinga ubeberu wa Magharibi kama vile Iran na vilevile washindani wakuu wa nchi hizo, yaani China na Russia. Na ndio maana nchi hizo, hususan Iran na China, huwa zinajibu mapigo kwa kuandaa na kutoa ripoti za kila mwaka za ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na Marekani; na kwa upande wa Iran ripoti hizo hujumuisha nchi mbili za Marekani na Uingereza.

Marekani na Uingereza zinajiona zina kinga inayozuia kuchunguzwa hali yao ya haki za binadamu, na kwa sababu hiyo, huwa hazijali hata kidogo ripoti, matamko na maazimio yanayotolewa na taasisi za haki za binadamu kama Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu katika nchi hizo, na hasa Marekani.

Uzandiki wa Marekani

Kwa mujibu wa ripoti ya ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa na Marekani mwaka 2024, katika mwaka huu unaomalizika, umeendelea kushuhudiwa ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa na Marekani katika ngazi ya kimataifa, uzandiki wa nchi hiyo wa kujionyesha kuwa ni kinara wa haki za binadamu duniani, kuzitumia haki za binadamu kama wenzo wa uingiliaji na wa kutoa ushirikiano kwa utawala wa Kizayuni katika kukiuka haki za binadamu za Wapalestina, kukiuka kimfumo haki za binadamu, kufanya jinai za mara kwa mara kwa ajili ya kuulinda mfumo wa ubaguzi wa rangi wa Apathaidi wa Kizayuni, kuendeleza hali ya kidhalimu ya kuchukua hatua za mabavu za upande mmoja dhidi ya nchi zingine na kuyapatia silaha na kuyaunga mkono makundi ya kigaidi. Aidha, uungaji mkono usio na masharti wala mpaka wa Marekani na nchi nyingine za Magharibi kwa utawala wa Kizayuni umeligeuza eneo la Asia Magharibi kuwa mahala penye hali mbaya zaidi duniani katika suala la ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa dhidi ya wananchi wa Palestina hususan wanawake na watoto, ambayo ni matokeo ya moto wa vita uliowashwa na utawala huo ghasibu.

Vilevile, kwa mujibu wa Ripoti ya Ukiukwaji wa Haki za Binadamu uliofanywa na Uingereza katika mwaka 2024 imeelezwa kuwa, hatua na vitendo vya serikali ya Uingereza vya kukiuka haki za binadamu katika ngazi ya ndani na kimataifa vinaendelea kukosolewa na taasisi za Umoja wa Mataifa za haki za binadamu, Baraza la Ulaya na watetezi wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na ukosoaji dhidi ya ubaguzi wa rangi wa kimfumo unaofanywa nchini Uingereza, ambao ni miongoni mwa matukio ya mara kwa mara ya ukiukaji wa haki za binadamu yaliyoshuhudiwa katika nchi hiyo.

Uingereza imekandamiza watetezi wa Palestina

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya kila mwaka, kadhia ya wazi zaidi ya ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa na Uingereza ni kuhusiana na Palestina. Kwa kuupelekea silaha utawala wa Kizayuni na kuuunga mkono kifedha, kiusalama na kiteknolojia, mbali na Uingereza kushirikiana na utawala huo ghasibu katika kuendelea kukiuka haki ya kuainishwa mustakabali wa watu wa Palestina, imekuwa na nafasi ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja pia katika kutenda jinai za kivita, jinai dhidi ya binadamu na jinai ya mauaji ya kimbari katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Kwa ujumla, tunapoiangalia hali ya haki za binadamu ya Marekani na Uingereza tutabaini kuwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu umefanywa na nchi hizo mbili. Kuendelea kuwepo miamala ya kibaguzi dhidi ya watu weusi na wasio wazungu, ukatili na ukandamizaji mkubwa unaofanywa na polisi wa Marekani dhidi ya watu hao, na vilevile rekodi chafu ya Washington nje ya Marekani kupitia operesheni za kijeshi, mashambulizi na jinai za kivita katika nchi nyingi kama vile Vietnam, Afghanistan, Iraq na Syria, kuanzisha magereza na kuamiliana na watuhumiwa inaowashikilia kwenye magereza hayo kama wanyama mbali na kuwatesa na kuwaadhibu, pamoja na kuiunga mkono kwa kila hali Israel katika mauaji ya kimbari ya Wapalestina, yote hayo yanathibitisha uongo wa madai ya Washington ya kutetea na kuunga mkono haki za binadamu. Nchini Uingereza nako, ubaguzi na ukatili dhidi ya wasio wazungu, wahamiaji na wanaotafuta hifadhi, kushamiri ubaguzi na ukatili dhidi ya Waislamu ambao wengi wao ni wahamiaji na waomba hifadhi, mazingira magumu na yasiyofaa yanayowakabili wafanyakazi wa vibarua, ubaguzi wa kijinsia na kikabila katika sekta mbalimbali hasa za ajira na elimu, na kutoa msaada mkubwa wa silaha kwa Israel ni miongoni mwa masuala ya wazi kabisa ya ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na serikali ya London.

4254284

Habari zinazohusiana
captcha