IQNA

Ibada ya Hija 1444

Vidokezo vya afya kwa ajili ya wanaoelekea katika ibada ya Hija

14:37 - June 05, 2023
Habari ID: 3477102
TEHRAN (IQNA) – Hija, ni ibada ya kila mwaka ya dini ya Kiislamu katika mji mtakatifu wa Makka, inakaribia kutufikia, na safari ya kiroho pia inahusisha maandalizi mazuri ya matibabu kwa uzoefu wa kufurahisha.

Mnamo mwaka wa 2019, kabla ya janga la COVID-19 kukumba ulimwengu, Mahujaji milioni 2.5 walishiriki katika ibada ya Hija. Mnamo mwaka wa 2020, ili kuzuia kuenea kwa virusi vya COVID-19, serikali ya Saudi iliweka marufuku ya Hija kwa Waislamu walioko nje ya Saudia na hivyo waliotekeleza Hija walikuwa ni wakaazi wa Saudi Arabia tena kwa idadi ndogo.

Huku vizuizi vinavyohusiana na COVID vikipunguzwa, Waziri wa Saudi wa Hajj na Umrah Tawfiq bin Fawzan Al-Rabiah alisema mnamo Januari kwamba ufalme huo umepanga kupokea Mahujaji milioni 2 wakati wa msimu wa Hija mwaka huu, kutoka 900,000 mwaka jana.

Waislamu wote, ambao wana uwezo wa kimwili na kifedha, wanatakiwa kufunga safari ya kwenda Makka kwa ajili ya Hija angalau mara moja katika maisha.

Ni muhimu kuwa na afya na nguvu ya kimwili wakati wa safari hii muhimu ya kiroho. Kuchukua tahadhari fulani za kiafya huwasaidia Mahujaji kuelekeza fikra zao zote katika ibada.

Walakini, mikusanyiko kama hiyo iliyojaa watu kawaida huleta hatari ya kuenea kwa haraka kwa magonjwa ya kuambukiza kama vile COVID-19 ambayo ilileta tishio kubwa kwa afya ya umma kote ulimwenguni.

Mbali na magonjwa ya kuambukiza, sumu ya chakula na kiharusi cha joto ni masuala mengine ya afya ambayo Mahujaji wanaweza kukumbana nayo wakati wa safari ya Hija.

Wale ambao ni wazee na walio na magonjwa sugu wanahitaji kuwa waangalifu zaidi ili kuzuia kuzorota hali yao ya kiafya.

Ni kwa msingi huo ndio maana mashirika ya afya hutoa mapendekezo ya kuzuia athari kwa afya ya umma ya kimataifa katika mikusanyiko mikubwa ya kila mwaka ulimwenguni, pamoja na ibada ya Hija.

Kwa sababu ya kufuata kalenda ya mwezi, misimu ya Hija inatofautiana. Kuanzia 2005 hadi 2013 safari ya Hija ilianguka katika msimu wa kabla ya baridi kali na msimu wa baridi kali na misimi hiyo huhusishwa na magonjwa ya msimu wa baridi na kadiri kalenda ya mwezi inavyoendelea sasa inafanyika katika miezi ya kiangazi wakati magonjwa tofauti yanatawala.

Serikali ya Saudi Arabia kila mwaka huchapisha mahitaji na kanuni rasmi za afya ili kuzuia na kudhibiti vitisho vya kiafya wakati wa Hija

Mwaka huu ushauri wa afya unajumuisha orodha ya chanjo za lazima na zinazopendekezwa kama vile meninjitisi ya meningococcal, COVID-19, polio, na MMR.

Ushauri huo unasema Mahujaji wanapaswa kufanya  mazoezi zaidi ya mwili wiki 4 hadi 6 kabla ya safari kwani Hija inaweza kuwa ngumu na inahusisha kutembea kwa kilomita nyingi.

Inapendekezwa pia kufanya uchunguzi wa jumla ili kuhakikisha afya yako nzuri.

Ushauri huo haswa unawaagiza Mahujaji walio na magonjwa yanayowalazimu kutumia dawa kila siku kuhakikisha kuwa  wanabeba kiasi cha kutosha cha dawa walizoandikiwa wakati wa safari.

Ili kuepuka ajali na majeraha, na pia kutochoka haraka inapendekeza kuvaa viatu vyepesi, na kuwa waangalifu zaidi unapotembea kando ya barabara zenye magari mengi, au karibu na msongamano mkubwa wa magari.

Saudi Arabia ina hali ya hewa kavu. Ili kuepuka hatari za kiafya zinazohusiana na hali ya hewa kama vile kuchomwa na jua, uchovu wa joto, kiharusi cha joto, na upungufu wa maji mwilini, Mahujaji wanapendekezwa kuchukua tahadhari zinazohitajika.

Kwa mfano ni bora kutumia mafuta ya kukinga ngozi na athari za jua kali, kunywa maji mengi, na kufanya baadhi ya ibada jioni ili kuepuka joto la mchana.

Usafi mzuri na kunawa mikono mara kwa mara ni mojawapo ya mbinu ya kupunguza hatari yako ya kupata na kueneza magonjwa kama mafua na COVID-19.

Ili kuzuia kuhara, pendekezo lilisema unahitaji kujiepusha na vyakula na vinywaji vilivyochafuliwa na uendelee kuosha mikono yako mara kwa mara, haswa kabla ya kula na kunywa.

Aidha ushauri huo unataka Mahujaji wajilinde dhidi ya kuumwa na mbu na wadudu wengine, kwani wanaweza kueneza magonjwa kama vile homa ya dengue na malaria.

Unaporudi nyumbani, inashauriwa uangalie dalili zozote hasa zinazohusishwa na maambukizi ili kupata matibabu mapema.

Kuzingatia afya yako wakati wa safari hii ya kipekee kunaweza kukusaidia kufurahiya sana ibada hii ya aina yake.

3483827

Kishikizo: Hija 1444 hija Afya
captcha