Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo Jumatano mjini Tehran wakati alipoonana na maelfu ya maveterani na wanaharakati wa Vita vya Kujihami Kutakatifu na Muqawama na amegusia hali iliyopo hivi sasa katika eneo hili na jinai za utawala wa Kizayuni huko Ghaza na Lebanon, pamoja na mapambano na kusimama kidete na kusisitiza kuwa, mfano wa mapambano hayo ni ile Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu wakati wa Vita vya Kujihami Kutakatifu (vita vilivyoanzishwa na utawala wa zamani wa Iraq dhidi ya Iran) na kusisitiza kuwa, licha ya kushuhudiwa matukio machungu ya jinai za utawala ghasibu wa Kizayuni huko Ghaza, Ukingo wa Magharibi na Lebanon, lakini mpaka hapa tulipofikia hivi sasa, ushindi ni wa kambi ya Jihadi katika Njia ya Allah na kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu ushindi wa mwisho utakuwa ni wa kambi ya Muqawama wa Palestina na Hizbullah ya Lebanon.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, nchi moja ya Kiislamu yaani Palestina inakaliwa kwa mabavu na kafiri khabithi zaidi duniani na hukumu ya wazi kabisa ya kisheria ni Waislamu wote kuungana na kufanya jitihada kubwa za kuikomboa Palestina na Msikiti wa al Aqsa.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameongeza kuwa, Hizbullah ya Lebanon ambayo imejitolea muhanga kwa ajili ya Ghaza na hivi sasa inavumilia matukio machungu, nayo imo kwenye Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia fedha nyingi, silaha na propaganda kubwa za maadui duniani na kusema kuwa, ni kweli zana na suhula za waumini na wanajihadi ni kidogo sana ikilinganishwa na upande wa adui, lakini washindi kwenye vita ni wanajihadi katika njia ya Allah yaani Muqawama wa Palestina na Hizbullah ya Lebanon.
3490040