IQNA-Khatibu wa Msikiti wa Al-Aqsa Sheikh Ekrima Sabri amesema, kauli aliyotoa hivi karibuni waziri wa usalama wa ndani wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Msikiti wa Al-Aqsa ni hatarishi.
Duru za Kiebrania zilitangaza hivi karibuni kuwa Itmar Ben Gvir, waziri wa usalama wa ndani wa utawala wa Kizayuni, anafuatilia kujenga sinagogi ndani ya Msikiti wa Al-Aqsa.
Kwa mujibu wa ripoti ya Al Jazeera, Sheikh Ekrima Sabri, Imamu wa Msikiti wa Al-Aqsa amesisitiza katika mahojiano na televisheni hiyo kwamba: Itmar Ben Gvir hana ushahidi wowote wa kuthibitisha madai yake kwamba Mayahudi wana haki kwenye Msikiti wa Al-Aqsa.
Sheikh Sabri amesema, mipango inayodaiwa na kufuatiliwa na Ben Gvir imefeli na kugonga mwamba na akatamka bayana: "tunasisitiza kuwa Msikiti wa Al-Aqsa ni wa Waislamu na tunatoa indhari dhidi ya kuukaribia".
Katika mahojiano hayo na Al Jazeera Imamu na Khatibu wa Msikiti wa Al-Aqsa amesema, miradi inayozungumziwa na utawala wa Kizayuni ni mipango hewa na ya udhanifu tu na kwamba Msikiti wa Al-Aqsa utabaki kuwa Msikiti wa Al-Aqsa; na akaongeza kuwa: mipango yao ni hewa na ya udhanifu; na baraza la mawaziri la Israel linabeba dhima kamili ya kitakachotokea dhidi ya msikiti huo.
Ikumbukwe kuwa, Msikiti wa Al-Aqsa, ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu na nembo kuu ya utambulisho wa Kiislamu na wa Palestina ulioko katika mji wa Baitul-Muqaddas, daima umekuwa ukiandamwa na vitendo vya hujuma na uharibifu vya utawala unaoikalia Quds tukufu kwa mabavu.
4233702